Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekwenda kwenye mstari wa mbele kuongoza vita dhidi ya wapiganaji wa Tigray.

Wanariadha Haile Gebrselassie na Feyisa Lilesa wamesema wako tayari kwenda mstari wa mbele katika vita dhidi ya vikosi vya waasi.

0
Abiy Ahmed, waziri mkuu wa Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekwenda kwenye mstari wa mbele wa mapigano ili kuongoza vita dhidi ya wapiganaji wa Tigray.

Abiy ataongoza vita kukabiliana na waasi wa Tigray, vita ambavyo vimedumu kwa mwaka mmoja sasa. Hatua yake imesababisha ongezeko la watu wanaojiandikisha kujiunga na jeshi la taifa linalokabiliana na waasi.

Naibu waziri mkuu Demekele Mekonnen Hassen atasimamia shughuli za kawaida za serikali wakati waziri mkuu hayupo.

Magwiji wa Olimpiki wa Ethiopia Haile Gebrselassie na mshindi wa medali ya fedha Feyisa Lilesa wamesema wako tayari kwenda mstari wa mbele katika vita dhidi ya vikosi vya waasi.

Haile Gebrselassie bingwa wa mbio za Olimpiki

Mataifa yenye nguvu zaidi duniani yameelezea hofu yao kuhusu ongezeko la watu wanaojiunga na mapigano hayo hatua ambayo inaweza kutatiza juhudi za kusitisha mapigano, huku waasi wakidai wanasonga mbele kuelekea mji mkuu Addis Ababa na serikali za kigeni kuwaambia raia wao kuondoka.

Siku ya Jumatano mamia ya wanajeshi wapya walishiriki katika hafla iliyofanyika kwa heshima yao katika wilaya ya Kolfe mjini Addis Ababa.

“Nilishangaa niliposikia” Abiy alipanga kuungana na majeshi kwenye vita, mmoja wa waliojisajili, Tesfaye Sherefa mwenye umri wa miaka 42 alisema.

“Kiongozi anapoondoka kwenye kiti chake, lengo lake si kuishi, bali ni kuinusuru nchi hii, nililia sana aliposema ‘nifuate’ na kwenda mstari wa mbele.”

Abiy alitangaza Jumatatu usiku mpango wake wa “kuongoza vikosi vya ulinzi” akiwa mstari wa mbele, lakini maafisa na vyombo vya habari vya serikali havijatoa maelezo kuhusu mienendo yake tangu wakati huo.

Waliosajiliwa kujiunga na jeshi la taifa kutoka Kolfe hata hivyo walitilia maanani azimio lake na wakavalia fulana zenye picha ya Abiy akiwa amevalia sare yenye maneno “Tuna jukumu la kihistoria kutetea jina huru la Ethiopia.”

“Ninajisikia mwenye fahari na ninasimama naye,” Esubalew Wale mwenye umri wa miaka 25 alisema baada ya kujiunga na jeshi.

Vita vya Ethiopia vilianza Novemba 2020 wakati Abiy alipotuma wanajeshi katika eneo la kaskazini la Tigray kupindua chama chake tawala cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2019 alisema hatua hiyo ilikuwa ni kujibu mashambulizi ya TPLF kwenye kambi za jeshi la shirikisho na kuahidi ushindi wa haraka, lakini kufikia mwishoni mwa Juni waasi walikuwa wameteka sehemu kubwa ya Tigray ukiwemo mji mkuu wa Mekele.

Tangu wakati huo TPLF imeingia katika mikoa jirani ya Amhara na Afar, na wiki hii ilidai kuwa imeteka mji ulioko kilomita 220 tu kutoka mji mkuu wa Addis Ababa.

Feyisa Lilesa bingwa wa mbio za olimpiki

Feyisa Lilesa mkimbiaji wa mbio za masafa marefu, aliviambia vyombo vya habari vya serikali kuwa kusonga mbele kwa waasi kunatoa “fursa nzuri”  ya kutetea nchi.

Mwanariadha huyo wa mbio za masafa marefu alipata umaarufu wa kisiasa baada ya kuonyesha mshikamano na kabila la Oromo waliouawa wakati walipokuwa wakipinga dhuluma zilizotekelezwa na TPLF wakati wa miongo mitatu ya utawala wake.

Katika mahojiano na vyombo vya habari vya serikali, Feyisa alisema anafurahia nafasi hiyo ya kupigana na TPLF yeye mwenyewe.

“Nchi inaposhambuliwa siwezi kusimama na kuangalia tu,” alisema Feyisa.

Ripoti tofauti ya vyombo vya habari vya serikali ilimnukuu bingwa wa mbio za masafa marefu  Haile Gebreselassie, akisema yeye pia, atapigana kwenye mstari wa mbele.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted