Wafungwa 38 wafariki na wengine 69 wajeruhiwa kwenye mkasa wa moto gerezani Burundi

“Tulianza kupiga kelele kwamba tutaungua, tulipoona moto unazidi kuwaka, lakini polisi walikataa kufungua milango,” - Mfungwa

0

Takriban watu 38 wamefariki dunia katika ajali ya moto iliyotokea katika gereza moja nchini Burundi. Makamu wa rais wa nchi hiyo, Prosper Bazombanza, anasema zaidi ya wafungwa wengine 60 wamejeruhiwa katika moto uliowaka katika gereza kuu la Gitega siku ya Jumanne.

Mfungwa mmoja alidai walinzi walisita kufungua seli moto ulipozuka. “Tulianza kupiga kelele kwamba tutaungua, tulipoona moto unazidi kuwaka, lakini polisi walikataa kufungua milango,” mfungwa huyo alisema.

Wale waliokuwa na majeraha mabaya walipelekwa hospitalini. Hii ni mara ya pili kwa moto kuzuka katika gereza hilo mwaka huu.

Mwezi Agosti wizara ya mambo ya ndani ilisema hitilafu ya umeme ilisababisha moto huo. Hakuna majeruhi walioripotiwa katika tukio hilo la mwezi Agosti.

Msongamano katika magereza ya Burundi

Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.

Hata hivyo, vyombo vya habari vya nchini vinaripoti zaidi ya wafungwa 1,500 walizuiliwa katika seli zilizostahili kushikilia wafungwa 400.

Ni tatizo la kawaida nchini. Mnamo mwezi Juni, wafungwa 5,255 walipata msamaha wa rais uliolenga kupunguza idadi ya wafungwa katika jela.

Wakati huo kulikuwa na karibu watu 13,200 katika magereza ambayo yalipangwa kushikilia wafungwa wasiozidi 4,100.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted