Dunia imerekodi idadi kubwa zaidi ya visa vya UVIKO 19 kwenye wiki moja

Zaidi ya visa milioni 6.5 vimeripotiwa kote duniani kati ya Desemba 22 na 28 2021

0

Zaidi ya visa milioni 6.5 vimeripotiwa kote duniani kati ya Desemba 22 na 28

Katika kipindi cha wiki saba, dunia imeweka rekodi ya juu ya maambukizi ya UVIKO 19 kuwahi kuripotiwa baada ya zaidi ya visa 935,000 kugunduliwa kila siku kati ya tarehe 22-28 Desemba, kulingana na hesabu za AFP.

Takwimu hizo, za juu zaidi tangu virusi hivyo kuibuka kwa mara ya kwanza mwishoni mwa 2019, zinatokana na hesabu inayotolewa kila siku na mamlaka za afya kutoka kila nchi.

Idadi kubwa ya visa hatari zaidi na visivyo na dalili bado vingali haviripotiwi licha ya watu wengi kupimwa virusi hivyo katika nchi nyingi tangu janga hilo kuanza.

Pia, sera ya kupima ugonjwa huo inatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.

Huku visa 6,550,000 kote duniani vikiwa zimerekodiwa kati ya Disemba 22 na 28 Desemba – ikiwa ni takriban visa 935,863 kwa siku — virusi hivyo vinaenea kwa kasi isiyokuwa ya kawaida.

Takwimu ni zaidi kuliko rekodi ya hapo awali kati ya tarehe 23-29 Aprili wakati visa 817,000 vilirekodiwa kila siku.

Maambukizi yaliyogunduliwa, ambayo yamekuwa yakiongezeka duniani tangu katikati ya mwezi Oktoba, yaliongezeka kwa asilimia 37 zaidi katika siku saba zilizopita.

“Kiwango cha ongezeko la maambukizi mapya na ya haraka kinaweza kuwa mchanganyiko wa kukosa kinga madhubuti mwilini na kuongezeka kwa uambukizaji wa kirusi cha Omicron,” Shirika la Afya Duniani lilisema Jumanne.

“Hatari ya jumla kuhusiana na kirusi kipya cha Omicron inasalia kuwa kubwa,” wakala wa afya wa Umoja wa Mataifa uliongeza.

Kwa sasa, mlipuko wa idadi ya visa vilivyogunduliwa haujasababisha kuongezeka kwa idadi ya vifo duniani, ambavyo vimekuwa vikipungua katika wiki tatu zilizopita.

Takriban vifo 6,450 vimerekodiwa kwa siku kwenye siku saba zilizopita, hii ikiwa ni kiwango cha chini kabisa tangu mwisho wa Oktoba 2020.

Katika kilele cha janga hili, vifo 14,800 vilirekokodiwa kila siku kati ya 20-26 Januari 2021.

Maambukizo mapya yanatokea Ulaya, ambapo zaidi ya visa milioni 3.5 vimerekodiwa katika siku saba zilizopita, ikiwa ni zaidi ya visa 510,000 kwa siku.

Kiwango hicho cha maambukizi pia hakijawahi kutokea, kwani bara halijawahi kurekodi zaidi ya visa 300,000 kwa siku katika mawimbi ya hapo awali.

Katika miaka miwili tangu virusi hivyo kugunduliwa, zaidi ya visa milioni 282 vya UVIKO-19 vimegunduliwa rasmi duniani, na vifo zaidi ya milioni 5.4.

Kwa kuzingatia idadi ya vifo vingi vilivyohusishwa na UVIKO-19, Shirika la Afya Duniani linakadiria idadi ya vifo inaweza kuwa mara mbili hadi tatu zaidi ya ilivyoripotiwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted