Tanzania: Nani kukalia kiti cha Uspika Tanzania?

Wenye misemo yao wanasema kwa sasa habari ya mjini ni kuhusu nani atakalia kiti cha Uspika wa bunge la Tanzania?

0
Steven Masele, aliyewahi kuwa Naibu Spika wa Bunge la Afrika

Mchakato huu wa kumpata atakae kikalia kiti hicho umekuja baada ya aliyekuwa Spika wa bunge hilo Job Ndugai kuachia ngazi kwa hiari yake kutokana na sintofahamu iliyotikisa kwenye vyombo vya habari kwa kauli alizozitoa mbele ya kadamnasi.

Siku za hivi karibuni Ndugai alijikuta anakalia kuti kavu baada ya kusema maneno ambayo hatma yake yalimfanya ajing’atue kwenye wadhifa wake kwa hiari yake kabla ya kupewa barua ama kuitwa ndani ya chama chake.

Kauli yake aliyoitoa mjini Dodoma kuwa hatua ya Tanzania kukopa madeni makubwa katika taasisi za kimataifa inaweza kusababisha nchi kuuzwa, iliibua mjadala mzito vijiweni na hata kwenye makundi ya mitandao kama ya Whatsup hususani yale ya WanaCCM wenyewe. 

Wengi wao waliitafsiri kauli yake kama ni ukosoaji wa hatua ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Ndugai alinukuliwa akisema “Juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika Ndugai na kuongeza kuwa

“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya kuongoza nchi.Hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii.”

Siku hiyohiyo ambayo Ndugai alitoa kauli hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alijibu hoja ya Ndugai pasipo kutaja jina na kusema kwamba serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya kuleta maendeleo hata kama kuna watu wanatoa kauli za kukatisha tamaa. Rais Samia Suluhu alisema nchi imekuwa ikikopa tangu utawala wa Awamu ya Kwanza na kushangaa kwamba inakuwaje watu wanahoji wakati huu.

Mzozo huo hivi sasa ndio umetoa mwanya kwa wengine kuwania kiti cha Uspika baada ya Job Ndugai kuona mambo yanazidi kumuendea kombo.

Chama cha Mapinduzi kilitangaza ratiba kwa wanachama wake wenye nia ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, mchakato ambao utadumu kwa muda wa siku 5 na baada ya hapo patafanyika mchujo kisha hatua ya mwisho ni kwa wabunge wa chama hicho kupiga kura ya kuidhinisha nani atakua mrithi wa Job Ndugai.

Zoezi la uchukuaji fomu kwa WanaCCM, lilianza jana Januari 10 na hadi sasa zaidi ya wanachama 10 tayari wameshajitokeza kuchukua fomu kuwania kinyang’anyiro hicho.

Waliochukua ni Dk Simon Ngatunga, Tumsifu Mwasamale, Merkion Ndofi, Dk Tulia Ackson, Godwin Kunambi na Abwene Kajula. Wengine ni Patrick Lubano, Stephen Masele, Hamidu Chamani, Joseph Msukuma na Goodluck Ole Medeye

Lakini je sifa za Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zipi?

Miongoni mwa sifa zilizotajwa katika Katiba, Spika anatakiwa kuwa raia wa Tanzania aliyetimiza miaka 21 na

  • Anayejua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza.
  • Mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
  • Awe ni miongoni mwa Wabunge waliochaguliwa.
  • Awe amedhaminiwa na chama chake

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted