Morocco: Mhadhiri kufungwa miaka miwili jela kwa kuhusika katika kashfa ya ngono

Unyanyasaji wa kijinsia umeenea sana Morocco lakini wanawake wanasitasita kuripoti kwa kuhofia kulipizwa kisasi au kudhuru sifa ya familia zao.

0

Mahakama ya Morocco Jumatano ilimhukumu mhadhiri wa chuo kikuu kifungo cha miaka miwili jela kwa tuhuma za kuwapa wanafunzi wa kike alama bora kwa kushiriki ngono nao, vyombo vya habari vya nchini vimeripoti.

Ilikuwa ni hukumu ya kwanza kama hii katika kashfa ya “ngono kwa alama bora”ambayo imetikisa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika tangu Septemba, wakati vyombo vya habari vya Morocco vilipokea uvujaji wa jumbe zinazodaiwa kutumwa kati ya wahadhiri na wanafunzi.

Mshtakiwa, mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Hassan I kilichoko Settat karibu na Casablanca, alipatikana na hatia ya “unyanyasaji wa kijinsia” vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Wahadhiri wengine wanne watafikishwa mahakamani Alhamisi 13 Januari kwa mashtaka sawia ya ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Msururu wa kashfa kubwa za unyanyasaji wa kijinsia umetikisa vyuo vikuu vya Morocco katika miaka ya hivi karibuni, lakini vingi havijawahi kufikishwa mahakamani au mtu yeyote kuhukumiwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema unyanyasaji wa kijinsia umeenea sana nchini Morocco lakini wanawake wanasitasita kuripoti kwa kuhofia kulipizwa kisasi au kudhuru sifa ya familia zao.

Mnamo mwaka wa 2018, baada ya miaka mingi ya mjadala mkali, Morocco ilibadilisha sheria yake ili wanyanyasaji wa kijinsia wakabiliwe na vifungo vya jela, lakini wengine wanahoji kuwa sheria bado inashindwa kuwalinda wanawake.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted