Morocco kumzika mtoto Rayan aliyefariki baada ya kutumbukia kisimani

Mazishi yake yatafanyika katika kijiji alikozaliwa cha Ighrane, katika milima ya Rif kaskazini mwa Morocco

0
Rayan mtoto aliyetumbukia kisimani

Morocco inajiandaa Jumatatu kumzika mtoto Rayan, mvulana mwenye umri wa miaka mitano ambaye alifariki akiwa amenaswa kwenye kisima licha ya operesheni ya uokoaji wa siku nyingi.

Hatima ya mtoto huyo ilivuta hisia za ulimwengu baada ya kuanguka kwenye kisima chenye urefu wa mita 32 (futi 100) kilichokauka Jumanne iliyopita, na kuzua hisia nyingi mtandaoni.

Mazishi yake yatafanyika katika kijiji alikozaliwa cha Ighrane, katika milima ya Rif kaskazini mwa Morocco ambako tukio hilo lilifanyika.

Siku ya Jumamosi usiku, umati wa watu ulishangilia kwa furaha wakati waokoaji walipomfikia Rayan baada ya shughuli ya usiku kucha ya kuchimba kisima hicho ili kumuokoa.

Lakini matumaini yaligeuka kuwa huzuni wakati habari zilienea kwamba uokoaji ulikuwa umechelewa, na Rayan alikuwa amekufa.

Habari hiyo ilitangazwa na baraza la mawaziri la kifalme la taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika, baada ya Mfalme Mohammed VI kuwapa wazazi na rambirambi zake.

“Tunamshukuru mfalme, mamlaka na wale wote ambao wametusaidia,” babake Rayan Khaled Aourram alisema Jumamosi jioni. “Mungu asifiwe, warehemu wafu.”

Mwili wa Rayan ulipelekwa katika hospitali ya kijeshi huko Rabat, kulingana na binamu yake, ingawa hakuna ripoti iliyotolewa ya kufanyika kwa uchunguzi wowote.

Juhudi za kumwokoa Rayan zilifuatiliwa moja kwa moja duniani kote. Papa Francis, huku akiomboleza kifo cha mvulana huyo, alisifu jinsi watu wote walivyokuja pamoja kujaribu kumuokoa mtoto huyo.

Aourram alisema alikuwa akirekebisha kisima wakati mvulana huyo alipoanguka, karibu na nyumbani kwao.

Shimo hilo lenye upana wa sentimeta 45 (inchi 18) tu, lilikuwa jembamba sana kwa Rayan kufikiwa moja kwa moja, na kulipanua kulionekana kuwa hatari sana.

Raia wa Morocco walikuwa katika hali ya mshtuko baada ya taarifa za kifo cha mvulana huyo.

Mourad Fazoui kutoka mji wa Rabat aliita tukio hilo kuwa janga. “Roho yake ipumzike kwa amani na Mungu amfungulie milango ya mbinguni,” alisema mfanyabiashara huyo.

“Amewaleta watu pamoja,” mtumiaji wa Twitter alisema

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted