Vitoa machozi vyafyatuliwa dhidi ya waandamanaji Sudan

Maandamano yameitikisa nchi hiyo tangu mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan kuongoza unyakuzi wa kijeshi mwezi Oktoba

0

Vikosi vya usalama vya Sudan siku ya Jumapili viliwarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wakiandamana kupinga mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, wakati mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akiwasili nchini humo.

Maelfu ya watu waliandamana katika mji mkuu Khartoum, wakiwa wamebeba bendera za Sudan na mabango ya watu waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi katika miezi ya hivi karibuni.

Vikosi vya usalama vilifyatua gesi ya kutoa machozi na kuwajeruhi waandamanaji kadhaa waliokuwa wakielekea ikulu ya rais katikati mwa Khartoum.

“Tuko tayari kuandamana mwaka mzima,” alisema mwandamanaji mmoja, Thoyaba Ahmed mwenye umri wa miaka 24.

Maandamano ya mara kwa mara yameitikisa nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika tangu mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan kuongoza unyakuzi wa kijeshi mwezi Oktoba, na hivyo kuzua shutuma za kimataifa.

Hatua hiyo ilivuruga kipindi cha mpito kilichojadiliwa kwa uchungu kati ya viongozi wa kijeshi na raia kufuatia kuondolewa madarakani kwa rais Omar al-Bashir mwaka wa 2019.

“Tunataka kurekebisha hali ya nchi yetu ili kuwe na mustakabali mzuri,” muandamanaji Wadah Khaled aliambia AFP.

Takriban watu 81 wameuawa na mamia kujeruhiwa katika msako mkali dhidi ya maandamano hayo, kulingana na kundi huru la madaktari.

Tunahitaji kujitolea kutatua masuala ya nchi,” mwandamanaji mwenye umri wa miaka 25 Arij Salah alisema.

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Adama Dieng wakati huo huo anazuru Sudan hadi Alhamisi, katika safari iliyopangwa kufanyika mwezi uliopita lakini ikaahirishwa kwa ombi la mamlaka ya Sudan.

Makumi ya watu walikusanyika nje ya jengo la mahakama mjini Khartoum kupinga kesi ya watu kadhaa wa zama za Bashir.

Miongoni mwa waliofikishwa mahakamani ni waziri wa zamani wa mambo ya nje Ibrahim Ghandour, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kupanga mapinduzi mwaka wa 2020.

Familia ya Ghandour ilisema mwezi uliopita kwamba alikuwa ameanza mgomo wa kuto kula gerezani, pamoja na maafisa kadhaa wa serikali ya zamani.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted