Majaliwa:Tutaendelea kushirikiana na mataifa mengine kudumisha amani Afrika.

Waziri Mkuu wa Tanzania  Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha amani, ushirikiano, ustawi wa kijamii na kiuchumi unaendelea kushamiri katika nchi...

0
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye baada ya  kumalizika kwa mkutano wa kumi wa wakuu wa nchi wa Serikali zinazohusika na mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini DRC na kwenye ukanda wa maziwa makuu uliofanyika, jijini Kinshasa, DRC 

Waziri Mkuu wa Tanzania  Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha amani, ushirikiano, ustawi wa kijamii na kiuchumi unaendelea kushamiri katika nchi zote za Bara la Afrika.

Majaliwa amesema kuwa tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere Serikali ya Tanzania imeshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi barani Afrika, kutoa hifadhi kwa wakimbizi pamoja na kushiriki katika kazi ya kulinda amani.

Waziri Majaliwa jana alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano  wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Aidha amesema katika kuhakikisha inashiriki kwenye ukuzaji wa ustawi wa kiuchumi barani Afrika, Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kutoka uvinza (Tanzania)- Gitega (Burundi) hadi Kindu (DRC).

 Kadhalika, Majaliwa amependekeza kuwa katika mikutano mingine ya nchi wanachama wa Makubaliano ya Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC na Ukanda wa Maziwa Makuu Lugha ya Kiswahili iongezwe kama mojawapo ya lugha rasmi ya mikutano hiyo.

“Ni heshima kubwa sana kwa lugha yetu ambayo kwa sasa imepata idhini kutumika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”

Mkutano wa Kumi wa Wakuu wa Nchi na Serikali umepitisha Taarifa ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na pamoja na  maazimio yake. Mkutano wa Tisa ulifanyika Jijini Kampala, Uganda tarehe 08 Oktoba, 2018.

Mkutano huo umeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo baada ya kukabidhiwa Uenyekiti na Mwenyekiti wa sasa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa mkutano huo, Rais wa DRC, Tshisekedi alimshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Yoweri Museveni pamoja na viongozi wengine kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Kadhalika, kiongozi huyo ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na mtangulizi wake kwa faida ya DRC na Afrika kwa ujumla. Amesema viongozi hao wanaisadia nchi ya DRC katika kuimarisha ulinzi na Amani hususani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulizinduliwa nchini Ethiopia Februari 24, 2013 baada ya Wakuu wa Nchi 11 kusaini mkataba ulioanzisha mpango huo.

Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Angola, Afrika Kusini, Burundi, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kongo, Uganda na Zambia. 

Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Sudan zilijiunga na mpango huo Januari 31, 2014.

Mpango huo unalenga kusitisha mapigano Mashariki mwa DRC na maeneo mengine ya Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na kutoa majukumu kwa DRC kuimarisha usalama, nchi jirani kutoingilia masuala ya ndani ya DRC na kutounga mkono makundi ya waasi nchini humo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted