Tani ya cocaine iliyonaswa nchini Guinea-Bissau ‘yatoweka’ wasema polisi

Hali tete na umaskini vimeifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha ulanguzi wa cocaine kati ya Amerika Kusini na Uropa

0

Mkuu wa polisi nchini Guinea-Bissau alisema siku ya Alhamisi kwamba karibu tani moja ya cocaine iliyokamatwa na mamlaka mwishoni mwa mwaka jana ‘imetoweka’.

Domingos Monteiro, mkurugenzi wa polisi wa mahakama katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, alisema kuwa maafisa walikamata kilo 980 za cocaine mnamo Novemba 2021, katika operesheni ya magendo ambayo maelezo yake bado hayajafahamika.

‘Lakini kilo 975 zilitoweka’, mkuu wa polisi aliiambia AFP, akiongeza kuwa polisi na maafisa wa vikosi vya usalama wanashukiwa kuiba cocaine hiyo.

Afisa mmoja wa polisi amekamatwa, Monteio alisema.

Siku ya Alhamisi, kesi inayohusu usafirishaji haramu wa tani moja ya cocaine ilianza katika mji mkuu Bissau, mwandishi wa habari wa AFP aliyekuwepo alisema, ambapo washukiwa saba kati ya tisa walifikishwa mahakamani.

Guinea-Bissau ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, na imekuwa na historia ndefu ya mapinduzi ya kijeshi na mauaji ya kisiasa tangu uhuru wake kutoka kwa Ureno mwaka 1974. Mwezi huu ulishuhudia jaribio la mapinduzi lililotibuka dhidi ya Rais Umaro Sissoco Embalo.

Hali tete na umaskini vimeifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha ulanguzi wa cocaine kati ya Amerika Kusini na Uropa, huku viongozi wakuu katika vikosi vya usalama nchini humo wakihusishwa na biashara hiyo.

Mnamo Septemba 2019, polisi walikamata tani mbili za cocaine ambazo ziliwasili nchini Guinea-Bissau kutoka Colombia – usafirishaji mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted