Mahakama yafuta kesi tano za Ugaidi

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

0

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imefuta kesi tano za ugaidi na kuwaachia huru kwa masharti washtakiwa 12, waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kujihusiaha na vitendo vya ugaidi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Washtakiwa hao  Seif Mwishehe, Yusuph Rajabu, Buheti Buheti, Juma Athuman, Ally Nassoro maarufu kama Omary Swala, Hassan Mnele na wenzao sita.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hizo umetolewa mbele ya Mahakimu watano tofauti, ambao ni Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi, Huruma Shahidi na Yusto Ruboroga, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Jopo la mawakili wanne wa upande wa mashtaka likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Waziri Magumbo akisaidiana na Ramadhani Kalinga, Ashura Mzava na Yusuph Avoid, wameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hizo zimeitwa kwa ajili ya kutajwa na lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP), hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa hao.

Kwa mujibu wa wakili Magumbo washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 , iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao Desemba 23, 2015 na mwaka 2016 katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo, Dar es Salaam na eneo la Manyovu mkoani Kigoma.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted