Mbowe:Mimi nilikuwa naomba msifute mashtaka haya hadi ukweli udhihirike

Mbowe amesema alitamani sana kuona ukweli unadhihirika katika kesi hiyo kwani alitaka kuona wale walomtuhumu kwa kesi hiyo kuona watatoa ushahidi gani ambao utaidhihirishia dunia kwamba kweli yeye...

0

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe amesema Watanzania wengi wakiwamo viongozi wa dini na wa vyama vya  siasa walikuwa wanaomba mara kwa mara kuwa kesi hiyo ifutwe, lakini yeye mara zote alikuwa anaomba isifutwe hadi ukweli udhihirike.

Mbowe ameyasema hayo jana Jumapili akiwa kwenye ibada  katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania jijini Dar es Salaam alipokwenda kutoa shukrani.

Mbowe alisema: “Watu wengi walikuwa wanaomba mara kwa mara mtoeni Mbowe futeni mashtaka, lakini mimi mwenyewe nilikuwa naomba yasifutwe hadi ukweli udhihirike.”

Mbowe amesema alitamani sana kuona ukweli unadhihirika katika kesi hiyo kwani alitaka kuona wale walomtuhumu kwa kesi hiyo kuona watatoa ushahidi gani ambao utaidhihirishia dunia kwamba kweli yeye ni gaidi.

“Nilitamani nisikie hao walionituhumu kwa ugaidi watatoa ushahidi upi ili dunia ielewe kwa sababu kulikuwa na mahakama ya mahakamani na mahakama ya umma.”- Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA, 

Aidha Mbowe amesema hakuwahi kuuzunika wakati alipokuwa gerezani kwani akiwa huko kumekuwa na miujiza mingi imefanyika, lakini pamoja na hayo ameweza kujifunza mengi. 

“Watu wamelia, nimeona machozi mengi, nimeona furaha na vicheko vingi, lakini miezi 8 haikupotea bure nimepata muda mwingi wa kusoma wa kuandika na nilikua na amani kuliko nyinyi mlivyokuwa mnadhani, nilikuwa na furaha wakati wote kwa sababu hakika ni miujiza mingi imefanyika wakati mimi niko gerezani”- amesema Freeman Mbowe.

Kauli za mbowe zimekuja ikiwa ni siku ya tatu tangu alipoachiwa huru yeye na wenzake watatu, baada ya kufutiwa kesi ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili.

Katika hotuba yake Mbowe alipokuwa kanisani pamoja na mambo menginea alisema kuwa wakati akiwa magereza alikuwa kwa siku anapokea wageni zaidi ya 200, walikuwa wanafika kumjulia hali pamoja na kuzungumza mambo mengine, jambo ambalo lilimpa faraja zaidi.

“Ilikuwa nikianza saa tatu asubuhi mpaka saa tisa tunapofungiwa nakuwa na mgeni mmoja baada ya mwingine ikalazimika kuweka kumbukumbu ya mahudhurio kwa wageni wote wanaokuja kunipa pole watu wamelia na mimi nimeona machozi mengi furaha na vicheko vingi,” alisema Mbowe.

“Watu walikuwa wanatoka Kigoma kwa mabasi tena ya kukodi kuja kuniona wengine Kagera, Kyela lakini niseme ukweli baba mchungaji kuna wakati nilikuwa najiuliza mtu fulani sijamuona na fulani kaja mara moja lakini jana nilipata faraja baada ya kuja askofu mmoja na wachungaji nyumbani kufanya sala ya familia,”.

“Baba askofu aliniambia yawezekana nitakuwa najiuliza kwanini fulani hakuja kuniona nikiwa gerezani au kwanini fulani hakuja vya kutosha waliniambia nisifanye kosa hilo kwani kila aliyekuja kuniona alipewa kibali na Mungu na kuna mamia ambao hawakuja kwa sababu mbalimbali,” ameeleza

Freeman Mbowe aliachiwa huru na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa Machi 4,2022 baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Kesi hiyo ilifutwa baada ya siku 216 kupita tangu ilipoanza kusikilizwa Jumanne ya Agosti 31, 2021 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wengine waliofutiwa mashtaka hayo kwenye kesi hiyo ni Halfan Bwire, Adam Kasekwa, na Mohamed Ling’wenya, ambao waliwahi kuwa watumishi wa JWTZ kikosi cha KJ92, Ngerengere mkoani Morogoro waliofukuzwa kazi kutokana na makosa ya kinidhamu

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted