Ukraine yakataa kutoa njia salama kwa Urusi kwa wakimbzi wanaotoroka mashambulizi

Vladamir Putin ameahidi atatimiza lengo lake kwa njia yoyote ile iwe “kwa mazungumzo au kupitia vita”

0
Wakimbizi wakisubiri kuabiri basi katika mpaka wa Ukraine na Poland mnamo Machi 6. Zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 wamekimbia mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine tangu mashambuli hayo yalipoanza. (Photo by Louisa GOULIAMAKI / AFP)

Ukraine ilitupilia mbali pendekezo la Moscow la kuweka njia za kuwasaidia wakimbizi kutoka miji kadhaa iliyoshambuliwa na mabomu nchini Ukraine siku ya Jumatatu baada ya kubainika kuwa baadhi ya njia zingewaongoza wakimbizi kuingia Urusi au Belarus.

Pendekezo la Urusi la kuweka njia salama kutoka Kharkiv, Kyiv, Mariupol na Sumy limekuja baada ya raia wa Ukraine waliojawa na hofu kushambuliwa katika majaribio ya hapo awali ya kusitisha mapigano.

Urusi ilifanya mashambulizi ya zaidi usiku kucha wa kutoka angani, nchi kavu na baharini, na kuzidisha maafa ya kibinadamu ambayo yamesukuma zaidi ya watu milioni 1.5 kuvuka mipaka ya Ukraine na kuingia nchi jirani.

Vikwazo vya kimataifa vilivyokusudiwa kuiadhibu Moscow hadi sasa havijasaidia sana kupunguza uvamizi huo, na Washington ilisema sasa inajadili kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi na Ulaya.

Bei ya mafuta ilipanda hadi kufikia kiwango cha juu katika kipindi cha miaka 14 ,bei ya gesi pia ilipanda huku masoko ya hisa yakiporomoka na wawekezaji wakiwa na wasiwasi kuhusu kuzorota kwa uchumi wa dunia.

Matukio ya kutisha mwishoni mwa juma yalionyesha raia wa Ukraine wakiuawa walipokuwa wakijaribu kukimbia miji mbalimbali.

Wizara ya ulinzi ya Moscow mapema Jumatatu ilitangaza mipango mipya ya kuweka njia salama za kuwasidia wakimbizi kuhama Ukraine.

Lakini njia kadhaa zilielekea Urusi au mshirika wake Belarus, na kuzua maswali juu ya usalama wa wale ambao wanaweza kuzitumia njia hizo kuihama Ukraine.

“Hili si chaguo zuri kwa wakimbizi”, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk alisema.

Raia “hawaendi Belarusi na kisha kuchukua ndege hadi Urusi”.

Moscow ilisema uamuzi huo ulichukuliwa baada ya “ombi binafsi” la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye alizungumza na Vladimir Putin wa Urusi siku ya Jumapili.

Ofisi ya Macron hata hivyo ilikanusha kuwa kulikuwa na ombi kama hilo.

Wamekosa utu

Waandishi wa habari wa AFP waliona maelfu ya raia mapema Jumatatu wakikimbia mapigano kupitia njia isio rasmi huko Irpin, kitongoji cha kimkakati magharibi mwa Kyiv.

“Nina furaha sana nimefaulu kutoka,” alisema Olga, mwanamke mwenye umri wa miaka 48.

Watoto na wazee walibebwa kwenye mazulia yanayotumiwa kama machela kwenye njia, ambayo inaelekea juu ya daraja la muda na kisha kupitia njia moja iliyolindwa na jeshi na watu wa kujitolea.

Watu waliokata tamaa waliacha masanduku mazito ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuingia kwenye mabasi kutoka eneo la vita.

Siku moja kabla hapo familia ya watu wazima wawili na watoto wawili waliuawa kwa kilipuzi walipokuwa wakijaribu kuondoka eneo hilo lenye vita katika matukio ambayo yaliogopesha dunia.

“Hao wamekosa utu. Irpin iko vitani, Irpin hajajisalimisha, meya Oleksandr Markushyn alisema kwenye Telegram, akiongeza kuwa aliona kwa macho yake mwenyewe familia moja ikiuawa.

Majaribio mawili ya hivi majuzi ya kuruhusu raia wapatao 200,000 kuondoka kwenye bandari muhimu ya Azov huko Mariupol, ambako Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilionya kuhusu “matukio mabaya ya mateso dhidi ya binadamu,” pia yameishia katika maafa.

Familia moja ambayo ilifanikiwa kuondoka jijini ilieleza kukaa kwa wiki bila umeme na kukosa chakula na maji.

“Barabarani, tuliona kuna miili kila mahali, Warusi na Waukraine … tuliona kwamba watu walikuwa wamezikwa kwenye vyumba vyao vya chini.”

Hakukuwa na kusitishwa kwa mashambulizi yaliyotokea usiku wa kuamkia Jumatatu, huku ving’ora vya anga vikilia katika miji nchini kote, na mashambulizi makali ya angani katika mji wa pili wa Ukrainia Kharkiv, ambao umestahimili mashambulizi yasiokoma katika siku za hivi karibuni.

“Adui anaendelea na operesheni ya mashambulzi dhidi ya Ukraine, akilenga kuizingira Kyiv, Kharkiv, Chernihiv, Sumy na Mykolayiv,” mfanyikazi Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine alisema katika taarifa.

Meya wa Gostomel, mji ulio kaskazini mwa Kiev ambao ni nyumbani kwa uwanja muhimu wa ndege wa kijeshi, alipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya Urusi pamoja na watu wengine wawili wakati “alipokuwa akisambaza mkate kwa wenye njaa na dawa kwa wagonjwa,” maafisa wa eneo hilo walisema.

Miili ya watu tisa — raia watano na wanajeshi wanne — ilipatikana kwenye vifusi vya uwanja wa ndege wa Vinnytsia katikati mwa Ukraine baada ya uwanja huo wa ndege kuharibiwa baada ya kushambuliwa na kombora la Urusi siku ya Jumapili, huduma za uokoaji zilisema.

Hata hivyo mji muhimu katika eneo la Kharkiv, Chuguiv, umetekwa tena katika mashambulizi ya vikosi vya Ukraine, Anton Gerashchenko, msaidizi wa waziri wa mambo ya ndani, aliandika kwenye Telegram.

Watu 10,000 wakamatwa nchini Urusi

Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky alitoa wito upya kwa nchi za Magharibi kususia uuzaji wa mafuta na gesi kutoka Urusi.

“Ni vifo vingapi na hasara kiasi gani ifanyike ndio hatua ya  kulinda anga juu ya Ukraine ichukuliwe?”

Mapigano ya siku kumi na mbili yameua mamia ya raia na maelfu kujeruhiwa.

Maelfu ya watu — wengi wao wakiwa wanawake na watoto — wameingia katika nchi jirani katika kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro wa wakimbizi unaokua kwa kasi zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Washirika wa Magharibi wameweka vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa dhidi ya wafanyabiashara, benki na mabilionea kwa nia ya kuusonga uchumi wa Urusi na kuishinikiza Moscow kusitisha shambulio lake.

Lakini Rais wa Urusi Vladimir Putin amelinganisha vikwazo vya kimataifa na tangazo la vita dhidi yake na kuonya kwamba Kyiv “inatia shaka mustakabali wa serikali ya Ukraine” kwa kuendelea kupinga mabadiliko.

Moscow imelazimika kuzuia uuzaji wa bidhaa muhimu ili kupunguza uuzaji katika masoko bandia, huku siku ya Jumapili kampuni kubwa ya malipo ya American Express ilisitisha shughuli Urusi, siku moja baada ya Visa na MasterCard kutangaza hatua kama hizo.

Kampuni kubwa ya kupeperusha filamu kupitia mtandao ya Netflix ilisitisha huduma yake nchini Urusi huku TikTok mtandao wa kijamii ikisimamisha uchapishaji wa video mpya kutoka Urusi.

Licha ya adhabu kali kwa wale wanaopinga mashambulizi hayo, maandamano nchini Urusi dhidi ya uvamizi wa Ukraine yameendelea, huku zaidi ya watu 10,000 wakikamatwa tangu mashambulizi hayo kuanza.

Putin aahidi kutimiza lengo lake

Putin ameahidi atatimiza lengo lake kwa njia yoyote ile iwe “kwa mazungumzo au kupitia vita” na matarajio yanasalia kuwa madogo kwa duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu.

China ilisema Jumatatu ilikuwa tayari kusaidia upatanishi wa amani, na ikasisitiza kwamba urafiki kati ya washirika wa karibu Beijing na Moscow uko imara.

Wakati huo huo Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilianza kusikiliza rufaa ya Ukraine ya kuitaka Urusi kusitisha mapigano, lakini Moscow ilikataa kuhudhuria kikao cha mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa mjini The Hague.

Washirika wa NATO hadi sasa wamekanusha wito wa Ukraine wa kuzuia ndege za kijeshi kuruka katika anga za Urusi huku seneta mmoja mkuu wa Amerika, Marco Rubio, akisema Jumapili kwamba inaweza kusababisha “Vita vya Tatu vya Dunia” dhidi ya Urusi yenye silaha za nyuklia.

Putin ametishia “majanga makubwa na sio tu kwa Uropa bali pia ulimwengu mzima” iwapo ndege zake za kijeshi zitazuiwa kuruka katika anga za Urusi.

Kyiv pia imezitaka nchi za Magharibi kuongeza usaidizi wake wa kijeshi nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Antony Blinken alisema Washington ilikuwa “ikifanya kazi kikamilifu na Poland kuipatia Ukraine ndege za Amerika.

Moscow pia imewaonya majirani wa Ukraine dhidi ya kuwa mwenyeji wa ndege ya kijeshi ya Kyiv, ikisema kuwa wanaweza kuishia kuhusika katika mapigano ya kivita.

Silaha, risasi na fedha zimepelekwa nchini Ukraine kutoka kwa washirika wa Magharibi wakitaka kuimarisha Kyiv.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted