Tahadhari ya homa ya Manjano yatolewa Tanzania

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa tahadhari ya kuzuka kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano (Yellow Fever) ambapo amesema tarehe 03 Machi 2022, Wizara ya Afya...

0
Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa tahadhari ya kuzuka kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano (Yellow Fever) ambapo amesema tarehe 03 Machi 2022, Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka WHO hapa nchini ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano nchini Kenya.

Waziri Ummy amesema hadi kufikia tarehe 03 Machi 2022 nchini Kenya kulikua na wagonjwa wa Homa ya manjano 15 na vifo vitatu (3), aidha katika sampuli sita zilizopimwa maabara ya Kenya kwa kutumia vipimo vya serology na PCR sampuli 3 zilithibitika kuwa na maambukizi.

“Hapa nchini taarifa ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa zinaonesha kuwa hakuna taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya manjano, pia taarifa za ufuatiliaji wa tetesi za magonjwa haujaashiria kuwepo kwa ugonjwa huo”.amesema Waziri Ummy.

Aidha ameagiza Hospitali zote za Rufaa nchini kuwa na huduma za kupima na kutoa chanjo ya homa ya manjano kwa wasafiri na wenye uhitaji na pia ameagiza maafisa wa afya mipakani kuhakikisha wasafiri wanaoingia kutoka nchi zenye maambukizi wanakua na vyeti vya chanjo.

Waziri Ummy amewataka wananchi kuchukua tahadhari, na kujua dalili za ugonjwa wa homa ya manjano kama homa, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted