Tanzania yaahidiwa kupewa Euro milioni 25 kutoka Serikali ya Ubelgiji

Serikali ya Ubelgiji imeahidi kuipatia Tanzania Euro milioni 25 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 62, kwa ajili ya kutekeleza program mpya ya maendeleo ya miaka mitano katika...

0
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji nchini, Bw. Koenraad Goekint, mara baada ya kikao kilichofanyika Wizarani, jijini Dodoma

Serikali ya Ubelgiji imeahidi kuipatia Tanzania Euro milioni 25 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 62, kwa ajili ya kutekeleza program mpya ya maendeleo ya miaka mitano katika sekta ya elimu, inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka 2027, katika mkoa wa Kigoma.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL, Bw. Koenrad Goekint aliyeongoza ujumbe wa watu 7 kutoka nchini Ubelgiji walipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu MKuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba.

Bw. Goekint alisema kuwa Programu hiyo itajikita katika kuendeleza sekta ya elimu kwa kuangazia maeneo ya ukuzaji ujuzi wa ajira na utaalam kwa vijana hususani masuala ya uanagezi na ujasiriamali kwa lengo la kuzalisha ajira, kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kukuza zaidi ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za maendeleo na kuboresha masuala ya usawa wa kijinsia

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL kwa kuja na Program hiyo itakayotoa matokeo mazuri kwa kugusa maisha ya wananchi wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo.

“Program hii itakayotekelezwa mkoani Kigoma itagusa maenneo ya kipaumbele yaliyoainishwa kwenye utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), wenye lengo la kuboresha huduma za jamii, maisha ya watu na elimu ni moja ya maeneo hayo” alisema Bw. Tutuba.

Tutuba aliiomba Serikali ya Ubelgiji kupitia Shirika lake la Maendeleo-ENABEL, kuangalia uwezekano wa kuongeza maeneo mengine ya kimkakati ya kuboresha maisha ya wananchi ikiwemo huduma za afya na maji kwani wanawake ndio walengwa wakuu na ndio wanaokabiliana na changamoto ya uhaba wa maji.

Aidha, aliishauri Serikali ya Ubelgiji kupitia Shirika hilo kutekeleza mradi kama huo kwa upande wa Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wa Visiwa hivyo kufurahia matunda mazuri ya uhusiano mwema uliopo kati ya Tanzania na Ubelgiji.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, alisema kuwa kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Ubelgiji na ni matokeo chanya ya ziara ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyofanya nchini Ubelgiji tarehe 14 hadi 19 Februari 2022.

Akiwa nchini Ubelgiji, Rais Samia alikutana kwa mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, ambapo Viongozi hao walikubaliana kuweka mikakati ya kufanyika kwa majadiliano ya programu ya maendeleo na kuhakikisha kuwa mchakato wa maandalizi unakamilishwa kwa wakati.

Balozi Nyamanga alifafanua kuwa Tanzania imeingia katika orodha ya nchi 15 pekee duniani, ambazo Ubelgiji inaendesha program kama hizo jambo ambalo ni ishara ya mafanikio makubwa ya uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na alitoa wito kwa taasisi zote zitakazo kutana na ujumbe huo wa Ubelgiji hapa nchini kuweka kipaumbele mahitaji ya nchi katika eneo husika.

Ujumbe huo Shirika la Maendeleo la Ubelgiji-ENABEL unajumuisha watu saba na upo nchini kuanzia tarehe 7 hadi 18 Machi 2022, ambapo watafanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi za Serikali kuhusu maandalizi ya programu mpya ya ushirikiano.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted