Urusi inaishutumu Amerika kwa kufadhili utafiti wa silaha za kibiolojia nchini Ukraine

Washington na Kyiv kwa pamoja zimekanusha kuwepo kwa maabara zinazokusudiwa kuzalisha silaha za kibiolojia nchini humo.

0
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov “AFP PHOTO / Russian Defence Ministry”

Urusi siku ya Alhamisi iliishutumu Amerika kwa kufadhili utafiti katika utengenezaji wa silaha za kibiolojia nchini Ukraine, huku Moscow ikiongeza juhudi zake ya kudhibiti miji muhimu ya Ukraine.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov alisema katika hotuba yake kwenye televisheni kwamba “lengo la utafiti huo — na utafiti mwingine wa kibayolojia unaofadhiliwa na Pentagon nchini Ukraine — ulikuwa kuanzisha utaratibu wa kueneza kwa siri vimelea hatari.”

Konashenkov alidai kuwa wizara hiyo imepata hati zinazoelezea shughuli za kijeshi za kibaolojia za Amerika nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na uhamisho wa bidhaa za biolojia za Ukraine nje ya nchi.

Alisema Washington “ilipanga kufanya utafiti juu ya vimelea vya magonjwa ya ndege, popo na aina ya nyoka” pamoja na homa ya nguruwe ya Afrika na kimeta.

“Kampuni ya Biolaboratories ilivyoanzishwa na kufadhiliwa nchini Ukraine imekuwa ikifanya majaribio ya sampuli za virusi vya corona,” Konashenkov aliongeza.

Washington na Kyiv kwa pamoja zimekanusha kuwepo kwa maabara zinazokusudiwa kuzalisha silaha za kibiolojia nchini humo.

Ukraine ni nchi ambayo imekabiliwa na mashambulizi ya Urusi na makumi ya maelfu ya wanajeshi tangu Februari 24.

Urusi mwaka 2018 iliishutumu Amerika kwa kufanya majaribio ya kibiolojia kwa siri katika maabara huko Georgia, jamhuri nyingine ya zamani ya Soviet, ambayo kama vile Ukraine inalenga kujiunga na NATO na Umoja wa Ulaya.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted