Nape:Rais Samia ameirudishia heshima Tanzania

Nape ametoa kauli hiyo leo wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia, iliyoingia madarakani Machi mwaka jana, kufuatia kifo cha aliyekuwa rais...

0
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania,  Nape Nnauye, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Tanzania imerudishiwa heshima yake duniani tofauti na uongozi uliopita.

Nape ametoa kauli hiyo leo wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia, iliyoingia madarakani Machi mwaka jana, kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo,  Hayati John Magufuli.

“Serikali inaendeleza mashirikiano baina ya nchi, kikanda na kimataifa, kati ya sekta ya mawasiliano kupitia tume za pamoja za mashirikiano pamoja na jumuiya za mashirika ambayo Tanzania ni mwanachama. Wote tutakubaliana tunaposema ameifungua nchi,” amesema Nape.

Nape amesema “ wako watu watauliza ni nini? Maana yake ameirudisha Tanzania kwenye heshima yake duniani. Amekwenda kuzungumza na wenzetu, hatuwezi kubaki kisiwa. Hatuwezi kubaki yetu, ametuunganisha na mafanikio yaliyopatikana kwenye hii tamethibitisha safari zake katika jumuiya za kimataifa ni muhimu.”

Nape amesema, kuimarika kwa mahusiano hayo, kumepelekea mashirika ya kimataifa kuiwezesha Tanzania kupata nafasi kwenye mabaraza ya maamuzi ya kimataifa, ikiwemo la Umoja wa Posta Afrika.

“Tumepewa majuumu ambayo hapo mwanzo haikuwa rahisi sana, sasa tumeaminiwa, tumerudi duniani na kuwemo kwenye vikao vya maamuzi vya mashirika makubwa duniani,” amesema Nape.

Akielezea mafanikio ya wizara yake, Nape amesema kumekuwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika sekta ya mawasiliano.

Nape amesema, takwimu zinaonesha sekta hiyo kati ya Machi 2021 hadi February 2022, laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 51.2 hadi 55, sawa na ongezeko la asilimia nane, huku akaunti za pesa kupitia simu za mkononi zikiongezeka kwa asilimia 19, kutoka milioni 27.3 hadi 32.7.

Aidha, idadi ya watumaiji wa mtandao imeongezeka kwa asilimia saba, kutoka milioni 28 hadi 30, huku watoaji huduma za miundombinu ya mawasiliano wakiongezeka kutoka 19 hadi 23, wakati watoa huduma za ziada wakiongezeka kwa asilimia 54, kutoka 66 hadi 102.

Katika hatua nyingine, Nape amesema Serikali imetumia shilingi bilioni 93.5 kwenye ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo ujenzi wa minara 12 kwenye maeneo ya mipakani na kupeleka huduma za mawasiliano kwenye Hifadhi ya Burigi Chato, mkoani geita.

Pia, fedha hizo zimetumika kupeleka huduma hizo kwenye ofisi 10 za halmashauri za wilaya, ujenzi wa minara 42 kwenye visiwa vya Zanzibar, kuongeza uwezo wa minara 127 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted