Amuua mkewe na mtoto wake kisa gunia 60 za mpunga

Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia kati ya wanandoa hao kugombania magunia 60 ya mpunga

0
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame

Jeshi la Polisi Mkoani Katavi linawashikilia watu wanne waliokiri kufanya mauaji katika matukio tofauti, akiwamo mmoja aliyemuua mke na mwanawe na kuitupa miili yao kwenye pori la Kalilankulukulu wilayani Tanganyika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa Habari, kuwa Dutu Danga (30) ambaye ni mume wa marehemu alifanya mauaji hayo kwa kushirikiana na Yussuph Muge (32).

 Amesema Machi 8, 2022 Polisi walipokea taarifa za kutoweka kwa mama na mtoto katika mazingira ya kutatanisha.

“Tulifanya upelelezi wa kina Machi 9, 2022 tuliwakamata watuhumiwa akiwamo mume aliyezaa na huyo marehemu, baada ya kuwahoji wote kwa pamoja walikiri kuua na waliwaongoza polisi kuonyesha walipofukia miili,”

Kamanda Makame amesema “Baada ya kufukua yalipatikana mabaki ya miili ya marehemu na chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia kati ya wanandoa hao kugombania magunia 60 ya mpunga,” amesema

Kamanda Makame amesema kuwa wanandoa hao wakikorofishana walikuwa wanashtakiana kwa ofisa mtendaji wa kijiji hicho na kutozwa faini mara kwa mara hivyo mume aliona njia pekee ya kuondoa tatizo ni kumuua mkewe na mtoto wake.

Pia, Kamanda Makame amesema katika tukio lingine mkazi wa Mtapenda wilayani Tanganyika, Pauline Shilinde ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali, ambapo watu wawili wanashikiliwa baada ya kukiri kuhusika na mauaji hayo.

“Tuliwahoji wamekiri kuhusika na tukio hilo tukikamilisha upelelezi tutawafikisha mahakamani,” amesema Kamanda Makame

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted