Shahidi wa sita kesi ya Sabaya aomba ulinzi akiwa gerezani, adai kuwa Sabaya ni mtu hatari

Amedai madai hayo jana mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati akijitetea

0

Shahidi wa 6 katika kesi ya Uhujumu Uchumi,Utakatishaji fedha haramu na kumiliki Genga la Uhalifu inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro,Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita,Watson Mwahomange(27) amedai kuwa Sabaya ni mtu hatari sana na katika Maisha yake yote aliyokuwa akiishi nayo ameishi kama mateka kufuatia vipigo alivyokuwa akivipata.

Mwahomange ambaye wakili wake,Fridorini Bwemelo alijitoa kumtetea katika kesi hiyo alidai hayo wakati akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha Patricia Kisinda na kusema kuwa anamfahamu Sabaya toka mwaka 2019 wakati akimpigia picha katika shughuli zake binafsi mbalimbali za kikanisa.

Shahidi huyo ambaye ni mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo alidai na kukiri kwenda katika gereji ya Mfanyabiashara Francis Mrosso januari 20 mwaka jana, baada ya kutumwa na Sabaya kwenda kutengeneza Pampu katika gereji ya mfanyabiasharahuyo na Pampu hiyo ililetwa na mtu mmoja ambaye hamjui jina akiwa katika gari aina ya Benz.

Shahidi huyo ambaye alitumia saa takribani 2.30 kujitetea mahakamani hapo alidai aliifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa kwa kuelekezwa na mtu huyo gereji ilipo kwani yeye alikuwa haijui gereji ya Mrosso na alifika hapo na kumkuta shahidi wa 4 wa Jamhuri na kuambiwa gharama zake ni shilingi 100,000, na alimjulisha Sabaya lakini alichoambuliwa ni kipigo na kufungwa pingu kama mateka alipokuja Jijini Arusha kwa madai kuwa ameongeza cha juu.

Alidai Sabaya na walinzi wake walikuja Arusha na yeye aliitwa na mshitakiwa wa tano katika kesi hiyo,Silverster Nyengu(26) kuwa Sabaya anamwita katika hotel ya Point Zone na alifanya hivyo baada ya nusu saa lakini alikutana getini na msafara wa magari yakiwa yanatoka na aliambiwa apande gari ya nyuma aina ya VX Masai na kujikuta akiwekwa chini ya ulinzi kwa madai kuwa amechelewesha msafara.

Mwahomange alidai kuwa Sabaya alimwambia ni kwa nini anaitwa haendi kwa muda muafaka na anaenda kwa muda anaotaka na baada ya hapo aliwakabidhi walinzi na kutolewa wenge(kipigo) na kufungwa pingu na kwenda hadi katika gereji ya Sabaya akiwa chini ya ulinzi hatua ambayo ilimsononesha sana.

Alidai walipofika gereji ya Mfanyabiashara Mrosso akiwa chini ya ulinzi wa walinzi wake wakiwa katika gari tatu moja ikiwa gari ya serikali aliyokuwa akiitumia kama Mkuu wa wilaya ya Hai waliegesha magari na kuingia ofisini kwa Mrosso na kuanza kumhoji kwa nini ametengeneza Pampu bila kutoa list ya mashine ya EFD, Shahidi wanne wa Jamhuri alidai siku hiyo mawasiliano ya Mashine hiyo haikuwa nzuri na kuungwa mkono na yeye hatua iliyomkera Sabaya.

Shahidi huyo alidai hakwenda benki ya CRDB Kwa Mrombo wala nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kesi ya kuunda genge la uhalifu na utakatishaji fedha haramu mashitaka hayo hayajui wala hakushiriki hivyo aliiomba mahakama kwa unyenyekevu Mkubwa kuyafuta na kumwachia huru kwa kuwa hakushiriki,hakuwepo na hajui chochote.

Aidha kabla ya kumaliza Ushahidi wake alimwomba Hakimu Kisinda na Mahakama yake kumpa ulinzi yeye akiwa gerezani kwani Sabaya ni mtu hatari sana ombi ambalo Hakimu alitoa maelekezo kwa Askari Magereza kuhakikisha hilo linafikishwa kwa Mkuu wa gereza Kisongo Arusha ili utekelezaji uweze kufanyika.

Mbali ya Sabaya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Enock Mnkeni(41) ,Watson Mwahomange (27) maarufu kwa jina la Malingumu, John Aweyo(45),Syliverster Nyegu (26) maarufu kwa jina la Kicheche ambaye pia ni Msaidizi wa Sabaya,Jackson Macha(29) na Nathan Msuya(31).

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted