Mahakama yaondoa kesi ya Nondo, baada ya DPP kutokuwa na nia ya kuendelea nayo

Nondo alikuwa anashtakiwa kwa makosa mawili, moja ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na mbili, kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga.

0

Mahakama ya Rufani nchini Tanzania, Masjala ya Iringa imeondoa kesi iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP).

Nondo alikuwa anashtakiwa kwa makosa mawili, moja ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na mbili, kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga.

Novemba 5,2018, Nondo aliachiwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya upande wa Jamuhuri kushindwa kuthibitisha makosa yaliyokuwa yanamkabili bila kuacha shaka yoyote.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliokuwa umempa ushindi Nondo.

Hata hivyo leo Jumatano Machi 23, 2022, kesi ilikuwa inafika mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa lakini Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe aliwasilisha ombi mahakamani kuwa DPP hana nia ya kuendelea na Rufaa hiyo.

Kesi hiyo iliyokuwa chini ya majaji watatu, Shaban Ally Lila, Ignas Paul Kitusi na Abrahamu Mwampash na imeondolewa chini ya kanuni namba 77, kanuni ndogo ya nne za kanuni za Mahakama ya Rufaa.

Nje ya Mahakama Nondo amemshukuru Mungu kwa kuwa yupo huru na ataendelea na kazi zake kama kawaida.

“Hii kesi haikuwa na ushahidi wowote, nashukuru Mungu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu iliona hakuna ushahidi wowote. Nashukuru leo kesi imeondolewa kwa hiyo nipo huru,” amesema Nondo.

Wakili wa kujitegemea aliyekuwa anamtetea Nondo, Jebra Kambole amesema wanashukuru kuwa upande wa Serikali imeona haina nia ya kuendelea na kesi hiyo iliyokaa muda mrefu.

Wakili wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Paul Kisabo amesema tangu Nondo alipokamatwa waliendelea kumtetea.“Watetezi wa haki za binadamu hatupaswi kukata tamaa kuwatetea wanaokabiliwa na kesi kama hizi, leo Nondo yupo huru,” amesema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted