Taifa Stars kuminyana na Sudan leo

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kuikabili Sudan, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopo kwenye...

0

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo itashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kuikabili Sudan, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopo kwenye kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA.

Akizungumza kwenye Mkutano na waandishi wa habari jana Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen alisema kwenye mchezo wa leo, kikosi chake kitakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji wake.

“Tumejiandaa vizuri kuikabili Sudan, lakini kikosi chetu kitakuwa na mabadiliko hatutokuwa na kiungo Feisal Salum kutokana na majeraha ya msuli wa ndani, lakini pia tutawakosa wachezaji wa Simba, ambao kocha wao aliomba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya US Gendamarie,” alisema Poulsen.

Kocha huyo raia wa Denmark alisema pamoja na kutokuwepo kwa nyota hao, lakini hakuna kitakachobadilika kwani ameita kikosi cha wachezaji 28 wenye uwezo mkubwa na atahakikisha anapanga timu yake kwa kubalansi ili kupata ushindi.

Poulsen alisema kwenye kikosi hicho kuna sura nyingi mpya na wengine ni vijana wadogo wenye vipaji vya hali ya juu, anaamini watatimiza vizuri majukumu aliyowapa na kuwafurahisha mashabiki watakaojitokeza kushuhudia mchezo huo.

“Wakati tanaingia kambini tulijiandaa kwa michezo mitatu ndio maana nikaita wachezaji wengi kwa lengo la kuwajaribu na kuwapa mazoea ya kucheza timu ya taifa, nafurahi kuona wachezaji wengi wapya wakifurahi kambini wanajichanganya na wenzao inaonesha namna kambi hii ilivyo kuwa na mafanikio bila kuangalia matokeo,” alisema Poulsen.

Kocha huyo alisema wapo wachezaji wameonesha kumfurahisha, akiwemo mshambuliaji, George Mpole, ambaye alimpa dakika chache kwenye mchezo uliopita dhidi ya Afrika ya Kati, lakini alicheza kwa kujituma na kufunga bao la tatu.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Sudan, Burhan Tia alisema anauchukulia mchezo huo kama kipimo kizuri kuelekea mechi za kufuzu fainali za Afcon na Chan.

Kocha huyo mzawa alisema Tanzania ni timu nzuri na hiyo imetokana na kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji na uzoefu mkubwa kutokana na ushiriki wa klabu ya Simba kwenye michuano ya Caf.

“Nadhani tumefanya maamuzi sahihi kuja hapa kucheza na Tanzania sababu tutapata mazoezi mazuri yatakayotusaidia kujua ubora wetu kabla ya mechi za mashindano zinazotukabili mbeleni,” alisema Tia.

Huo ni mchezo wa pili kwa wenyeji Taifa Stars baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Afrika ya Kati na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia saa 1:00 usiku huku kiingilio ikiwa ni shilingi 3,000 kwa mzunguko na 5,000 kwa VIP A na C.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted