Prof Ngowi na dereva wake kuagwa leo

Prof Ngowi na dereva wake walifariki dunia siku ya Jumatatu Machi 28,2022  kwa ajali ya gari iliyotokea Mlandizi mkoani Pwani walipokuwa safarini kwenda mkoani Morogoro.

0
Aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es salaam, Prof Honest Ngowi.

Miili ya wafanyakazi wawili wa Chuo Kikuu Mzumbe; Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Honest Ngowi na dereva wake Innocent Mringo, inatarajiwa kuagwa leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.

Prof Ngowi na dereva wake walifariki dunia siku ya Jumatatu Machi 28,2022  kwa ajali ya gari iliyotokea Mlandizi mkoani Pwani walipokuwa safarini kwenda mkoani Morogoro.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Mzumbe jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chuo hicho, Rose Joseph, alisema hafla ya kuaga miili hiyo imelenga kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao kama watumishi wa umma na vilevile kama wanataaluma.

Aidha baada ya kuaga miili hiyo, mwili wa Mringo utasafirishwa siku hiyo hiyo kwenda nyumbani kwao Marangu Mwika, Moshi kwa ajili ya maziko yanayotarajiwa kufanyika kesho Ijumaa April Mosi, 2022 huku mwili wa Prof. Ngowi ukitarajiwa kufanyiwa ibada ya kifamilia kesho na kisha majira ya  jioni utasafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Jumamosi kijijini kwao Singa Kati, Kibosho.

“Kama taasisi tumeamua kuwapa heshima ya kuwajumuisha pamoja kwa sababu wamepata ajali pamoja na kufariki dunia pamoja, ili baadaye tuzipe familia nafasi ya kuwaaga kipekee na baadaye wapumzishwe kwa amani,” alisema Rose.

Aliwashukuru watu wote waliofanya kazi kwa karibu na Prof. Ngowi na Mringo na kazi walizofanya wataendelea kuzienzi wakati wote na hazitakuwa bure.

Prof. Ngowi aliyekuwa mbobevu wa masuala ya uchumi na biashara, mbali na kutoa elimu hiyo darasani, alikuwa akielimisha jamii kupitia majukwaa mbalimbali na kwenye vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na chuo hicho kwa ajili ya kuaga miili ya wawili hao, shughuli ya kuaga itaanza majira ya 3:00 asubuhi hadi saa 8:20 mchana.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted