Treni ya umeme kutumia saa 6 Dar – Tabora

Treni zitakayotumia reli hiyo zitakuwa na mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa ambapo zitatumia saa sita kutoka Dar es Salaam hadi Tabora kwa treni ya abiria huku za...

0

Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Makutupora – Tabora chenye urefu wa kilometa 368 ambapo kilometa 74 ni njia za kupishana, unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi trilioni 4.606, huku ukitarajiwa kutumia mienzi 42 ya ujenzi ikiwemo miezi minne ya majaribio

Treni zitakayotumia reli hiyo zitakuwa na mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa ambapo zitatumia saa sita kutoka Dar es Salaam hadi Tabora kwa treni ya abiria huku za mizigo zikitembea kilometa 120 kwa saa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema hayo leo Aprili 12, 2022 katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo unaofanywa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa.

Amesema makadirio ya majaribio yanategemea kuwa muda wa chini sana utakuwa miezi minne, lakini yanaweza kwenda hadi zaidi ya miezi hiyo.

“Kwa hiyo tunategemea mradi huu unaoanza saa hizi, utakamilika Oktoba 2025, hii inajumuisha usanifu na ujenzi kwa mkandarasi. Wakati anasanifu kuna baadhi ya nyumba zitapitiwa ila wote watapatiwa haki zao,”

Amesema mkandarasi amashapewa aina ya reli ambayo inayohitaji na si yeye kuleta kile ambacho hakitakiwi.

“Itakuwa na vivuko vya kutengenisha reli na barabara kwa kuondoa muingiliano wa barabara na reli, hii ikiwa na maana kuwa ikiwa yeye atakuwa chini treni itapita juu au yeye akiwa juu treni itapita chini jambo hili litafanya usalama kuwa wa juu”

Katika ujenzi huo, madaraja makubwa 32 yanatarajiwa kujengwa na vivuko vya juu 12 na vya chini 15 huku vivuko vya watembea kwa miguu, mifugo na wanyama vikiwa 49.

Treni hiyo itakapoanza kazi itakuwa na vituo nane Manyoni, Itigi, Kazikazi, Tula, Malongwe, Gaweko, Igalula na Tabora.

“Niwaambie tu, hatujengi stesheni hapa Tabora, tutajenga ‘shopping mall’, sehemu ya maduka makubwa, migahawa, tutakuwa na sehemu ya wafanyabiashara wadogo. Nina imani kuwa pale ndiyo itakuwa sehemu mnakutania,” amesema Kadogosa.

Treni hiyo  ya kisasa ya umeme SGR itatumia saa sita kutoka Dar es Salaam hadi kufika mkoani Tabora badala ya zaidi ya saa 20 hadi 36 zinazotumiwa na treni za kawaida kwa sasa.

Kwa mujibu wa Kadogosa hadi sasa Serikali imetumia jumla ya shilingi trilioni 6.13 katika ujenzi huo wakati mradi wote kuanzia Dar utagharimu shilingi trilioni 14.72

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted