Bibi amuua mjukuu wake wa siku moja kisa ugumu wa maisha

Kamanda wa Polisi wa Mkoa humo, James Manyama amesema mtuhumiwa alifanya tukio hilo Aprili 9, mwaka huu, saa tano usiku katika Kijiji cha Uvinza Wilaya ya Uvinza mkoani...

0

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma nchini Tanzania linamshikilia Lenita Asheri (54) akituhumiwa kuhusika na kifo cha mjukuu wake wa siku moja ambaye ni mtoto wa binti yake Penina Yekonia, kwa madai kuwa almefanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa humo, James Manyama amesema mtuhumiwa alifanya tukio hilo Aprili 9, mwaka huu, saa tano usiku katika Kijiji cha Uvinza Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kamanda Manyama alisema kichanga hicho kilizaliwa na Penina Yekonia (20) ambaye ana matatizo ya afya ya akili na kwamba mtuhumiwa alieleza sababu ya kufanya kitendo hicho ni kuondoa mzigo wa kutunza mtoto aliyezaliwa kwa sababu mama mzazi wa marehemu hakuwa na uwezo wa kumtunza mtoto.

Alisema baada ya Yekonia kujifungua mtoto huyo akiwa amejifungulia nyumbani, mtuhumiwa alikichukua kichanga kilichozaliwa na kukinyonga shingo na baadaye kukitupa chooni ili kupoteza ushahidi, ambako Yekonia aliendelea kutoa damu nyingi na ndipo walipomchukua ili kumpeleka Kituo cha Afya Uvinza kwa matibabu.

Aidha, baada ya Yekonia kufikishwa Kituo cha Afya Uvinza, mhudumu wa kituo hicho, Osward Mbara (34), alimpokea na baada ya kumkagua aligundua alikuwa amejifungua na ndipo muuguzi huyo alitoa taarifa polisi kwa uchunguzi.

Kutokana na hilo, polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa ambako baada ya upekuzi walikuta nguo zenye damu na kufanya mahojiano zaidi yaliyowezesha mtuhumiwa kukiri msichana huyo alijifungua mtoto, lakini amemnyonga na kumtumbukiza chooni, ambako polisi walifukua na kukitoa kichanga hicho.

Pamoja na hali hiyo, akiwa Kituo cha Afya Uvinza, msichana huyo alijifungua mtoto mwingine ambaye polisi kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa Jamii wanashughulikia mipango ya kumpeleka Kituo cha Kutunza Watoto Matyazo.

Kamanda Manyama alisema pamoja na kumkamata bibi wa marehemu akiwa mtuhumiwa wa kwanza, pia inamshikilia Paulina Edward jirani na rafiki wa bibi huyo anayetuhumiwa kumsaidia kutekeleza mipango hiyo.

Mahojiano ya polisi yamebainisha mtuhumiwa Lenita ana watoto 11 wa kuzaa akiwamo huyo mwenye matatizo ya afya ya akili ambaye pia ana mtoto mwingine aliyezalishwa na baba asiyejulikana akiwa anatunzwa hapo nyumbani, hivyo bibi huyo analalamika kukabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na idadi kubwa ya watoto alionao huku kipato cha kuwatunza kikiwa hakitoshelezi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted