Mwili wa Padre aliyekutwa amefariki kwenye tanki kuzikwa Pugu

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa siku chache zilizopita na Chansela wa Kanisa Katoliki, Padre Vincent Mpwaji kesho kutakuwa na mkesha wa kumuombea Padre Kangwa katika Parokia ya Mbezi...

0

Mwili wa Padre wa Parokia ya Mbezi Mshikamano, Dar es Salaam, Francis Kangwa unatarajiwa kuzikwa Alhamisi wiki hii katika makaburi ya mapadre Pugu, Dar es Salaam. Mwili wa Padre Kangwa ulikutwa ndani ya tangi la kuhifadhia maji jirani ya nyumba ya mapadre wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, Posta jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa siku chache zilizopita na Chansela wa Kanisa Katoliki, Padre Vincent Mpwaji kesho kutakuwa na mkesha wa kumuombea Padre Kangwa katika Parokia ya Mbezi Mshikamano, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Msimamizi Mkuu wa shirika hilo Jimbo la Mashariki ya Afrika, Padre Aloysius Ssekamatte, Aprili 12, mwaka huu Padre Kangwa aliegesha gari lake kwenye nyumba za mapadre za Atiman, Dar es Salaam na akahudhuria misa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.

Alisema baadaye Padre Kangwa alishiriki chakula cha mchana na mapadre wengine katika nyumba ya mapadre ya Atiman na siku iliyofuata baada ya kutoonekana kwa muda mrefu alitafutwa kwa njia ya simu ila hakupatikana.

“Wakati tunamtafuta kwa simu gari lake lilikuwa limeegeshwa katika maegesho ya magari katika nyumba hizo za mapadre, hivyo mapadre wenzake walihisi huenda kuna kitu kimemtokea na wakaanza kumtafuta kwenye kila chumba katika nyumba hiyo na pia walikwenda katika hospitali mbalimbali,” alisema Padre Ssekamatte katika taarifa hiyo. Alisema siku iliyofuata wakati wanajiandaa kutoa taarifa polisi, waliukuta mwili wa Padre Kangwa kwenye tangi la maji kwenye nyumba hiyo ya mapadre.

Alisema kwa sasa wanasubiri taarifa ya uchunguzi wa polisi kuhusu kifo hicho na taarifa zaidi zitatolewa baada ya taarifa hiyo kupatikana. Shirika hilo limetoa pole kwa familia na jumuiya yote kwa tukio hilo na kuwataka waendelee kuomba na kumuombea Padre Kangwa.

“Hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, lakini tumuamini Mungu, tuache mapenzi yake yatimie, apumzike kwa amani Padre Kangwa,” alisema Padre Ssekamatte. 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea na ukikamilika taarifa itatolewa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted