Wasiojulikana wamuua kikongwe wa miaka 90 nchini Tanzania

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amethibitisha tukio hilo na kusema upelelezi unaendelea ili watuhumiwa wakamatwe.

0

Kikongwe wa miaka 90, bi Marieta Thomas ambaye ni Mkazi wa mtaa wa Mpanda hoteli katika Manispaa ya Mpanda, amefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amethibitisha tukio hilo na kusema upelelezi unaendelea ili watuhumiwa wakamatwe.

“Upelelezi wa awali unaonyesha tukio linahusishwa na imani za kishirikina, baadhi ya wanafamilia walimtuhumu marehemu kuwafanyia ushirikina, jambo ambalo halikubaliki kisheria tunaendelea kufuatilia,” amesema Makame.

Mjukuu wa marehemu, Rosemary Titus amesema bibi yake amekutwa ameuawa siku ya Aprili 18,2022 majira ya asubuhi na kusema kuwa Bibi huyo alikuwa akiishi mwenyewe na wao walikuwa wakimpelekea mahitaji.

“Nimepigiwa simu na dada yangu jana asubuhi akaniambia bibi ameuawa nilishtuka sana, nimekuja kweli amepigwa na kitu chenye ncha kali kisogoni, hakuna mgogoro wa kifamilia uliokuwepo,”amesema Rosemary

Jirani wa familia hiyo, Peter Mwita ameeleza kuwa alionana na bibi kizee huyo siku ya juzi jioni na wakati akionana nae hakuwa na tatizo lolote.

“Jana jioni kabla sijaenda lindoni nilimsalimia alikuwa amekaa hapa nje, nashangaa kusikia ameuawa lakini nadhani watazame vizuri labda kuna mgogoro wa kifamilia,” amesema Mwita.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mpanda hoteli, Christina Ibrahimu amekiri kupokea taarifa za tukio hilo baada ya kupigiwa simu na mwananchi wake majra ya asubuhi kwamba kwenye eneo lake yametokea mauaji.

“Nilikuja haraka nikashuhudia nilishtuka sana kwasababu haijawahi kutokea tukio la kinyama kama hili, nilimpigia simu polisi kata baadaye askari polisi wakaja wakaubeba mwili wa marehemu,”

“Kwakweli tumeumia sana kwasababu huyu bibi alikuwa na umri mkubwa sana kwanini wamfanyie ukatili huo hata kama ni imani za kishirikina, nalaani kitendo hiki,” amesema Christina.

Chanzo Habari Leo

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted