Ukaguzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuanza leo

Aprili 20 mwaka huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema ukaguzi huo pia utafanyika katika vituo binafsi vya afya.

0

Serikali ya Tanzania  kupitia Wizara ya Afya nchini humo  leo inatarajia kuanza kukagua vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aprili 20 mwaka huu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema ukaguzi huo pia utafanyika katika vituo binafsi vya afya.

Profesa Makubi alisema hayo Dar es Salaam wakati wa mkutano wa viongozi wa vyama vya kitaaluma vya afya.

“Awali tulikuwa tunakagua vigezo vya kuendelea kuwa hospitali au maabara inapima majibu yenye ubora na sasa wiki ijayo tutaanza na hospitali ya Muhimbili tunataka tukague ubora wa huduma kwa kushirikiana na utawala na vyama vya kitaaluma,”alisema na kuongeza kuwa ukaguzi huo utaainisha maeneo yanayolalamikiwa na wananchi.

“Lengo sio kufungia mtu ila ni kuboresha huduma kama kuna mapungufu tutamwambia arekebishe kama kuna mazuri tutampongeza ili aweze  kuendelea vizuri na watumishi wote watashirikishwa na kupewa mrejesho katika hilo zoezi,”alisema Profesa Makubi.

Alisema ajenda kubwa ya wizara ni kuboresha huduma kwa kujenga hospitali nyingi kwenye mikoa,wilaya, na hatimaye kiwango cha vijiji.

“Tunachoangalia sasa hivi ni ubora gani mwananchi anapata anapoenda kwenye huduma za afya kwa maana  ya kupokelewa kwa lugha nzuri na wahudumu, pili anaweza kusikilizwa na daktari vizuri kuanzia maelezo  pamoja na kupimwa.

“Tatu anapata vipimo kwa usahihi ,nne anapata dawa ambazo ameandikiwa na kama ameandikiwa operesheni kwa muda unaostahili bila kuchelewa mwisho mwananchi anahudumiwa  kwa muda mfupi,”alieleza.

Alisema wanataka kukomesha tabia ya  mwananchi kwenda kituo cha afya na kukaa kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 4 mchana  bila kupata huduma. 

Kuhusu suala la maadili kwa watumishi wa umma, alisema wapo wasiozingatia miongozo na maadili hivyo kuchafua taswira ya watumishi.

“Tumegundua kuna tatizo katika ufundishaji wa wanafunzi kwa baadhi ya vyuo vya afya, tutashirikiana na Wizara ya Elimu kurekebisha changamoto hizo ili kuweza kupata wataalamu wenye viwango ili kulinda maisha ya wananchi,”alisema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted