Waathiriwa wa mlipuko wa mafuta Nigeria kuzikwa kwa pamoja

Mamlaka ya Nigeria Jumatatu ilikusanya maiti za watu zaidi ya 100 waliokufa katika mlipuko uliotokea kwenye kiwanda haramu cha kusafishia mafuta kusini mwa nchi hiyo

0

Mamlaka ya Nigeria Jumatatu ilikusanya maiti za watu zaidi ya 100 waliokufa katika mlipuko uliotokea kwenye kiwanda haramu cha kusafishia mafuta kusini mwa nchi hiyo na kujiandaa kwa maziko ya umati baada ya ajali iliyoelezwa kuwa ‘janga.’

Mlipuko huo uliotokea Ijumaa jioni katika eneo kati ya majimbo ya Rivers na Imo ulikuwa moja wa matukio mabaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo ambalo wizi wa mafuta na usafishaji haramu umekithiri, na kusababisha hasara kubwa na uharibifu wa mazingira katika nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta ghafi barani Afrika.

Kuungua kwa mabomba ya mafuta  ni jambo la kawaida nchini Nigeria, kwa sababu ya matengenezo duni lakini pia kwa sababu ya wezi ambao huharibu laini ili kunyonya mafuta, kuyasafisha kwenye mitambo ya haramu na kuuza mafuta hayo kwenye soko kinyume cha sheria.

“Kufikia leo asubuhi, idadi ya waliofariki imefikia 110, huku wengine wengi walioungua wakipokea matibabu katika hospitali,” Ifeanyi Nnaji wa Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Dharura (NEMA) katika eneo hilo alisema.

Nnaji alisema waathiriwa hao waliungua kiasi cha kutotambulika, hivyo kuwa vigumu familia zao kutambua miili yao.

“Tumekusanya miili ya waathiriwa kwa ajili ya maziko ya watu wengi,” Nnaji alisema, na kuthibitisha kwamba mazishi yatafanyika Jumanne.

Alisema watu kadhaa walikuwa wamekusanyika katika eneo hilo kwa “biashara haramu” kabla ya mlipuko huo ulioteketeza zaidi ya 100 hadi kufa.

Magari yaliyoteketea na makopo yaliyotumika kuokota bidhaa ghafi na mafuta ya petroli yaliyoibiwa yalitapakaa katika eneo la mkasa, alisema.

Tukio la Ijumaa lilikuwa la hivi punde zaidi kuikumba nchi inayozalisha mafuta ya OPEC Nigeria, ambayo imetatizika kuvutia uwekezaji mpya kwenye nchi hiyo.

Mlipuko mbaya zaidi wa bomba nchini Nigeria ulitokea katika mji wa kusini wa Jesse mnamo Oktoba 1998, na kuua zaidi ya wanakijiji 1,000.

Mafuta yasiyosafishwa hutolewa na wezi kutoka kwa mtandao wa mabomba inayomilikiwa na makampuni makubwa ya mafuta na kusafishwa kinyume cha sheria kuwa bidhaa.

Mele Kyari, mkuu wa Kampuni ya Kitaifa ya Petroli ya Nigeria (NNPC), alisema mapema mwezi huu kwamba Nigeria inapoteza mapipa 250,000 ya mafuta ghafi kwa wezi wa mafuta kila siku.

Watu wengi katika delta ya Niger wanaishi katika umaskini ingawa nchi hiyo ndiyo mzalishaji mkubwa wa mafuta katika bara , ikizalisha chini ya mapipa milioni mbili kwa siku.

Mkazi wa eneo hilo Ferdinand Amanze alisema ukosefu wa kazi huwasukuma watu kuiba mafuta ghafi.

“Kiwango cha ukosefu wa ajira kiko juu sana katika serikali hii ya mitaa,” alisema, akiongeza kuwa makampuni ya mafuta hayafanyii vya kutosha kwa jumuiya zinazozalisha mafuta katika mikoa inayozalisha mafuta.

Idris Musa, mkuu wa Shirika la National Oil Spills Detection and Response Agency  linaloendeshwa na serikali, alisema uchunguzi unaendelea.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari siku ya Jumapili alielezea tukio hilo kama “ janga la kitaifa,” ofisi yake ilisema.

Wale wanaondesha kiwanda hicho haramu “lazima wote wakamatwe na wakabiliane na haki,” aliongeza.

Kiongozi wa vijana eneo hilo Anyaoke Bright alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia matakwa ya jamii katika maeneo ambapo mafuta yanazalishwa.

“Serikali na kampuni za mafuta zinapaswa kuchukua hatua haraka ili jambo la aina hii lisitokee tena.”

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted