Kikosi kazi cha Rais Samia kuanza kupokea maoni ya wadau leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dodoma na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia kwa Katibu wa Kikosi Kazi hicho, Sisty Nyahoza, leo wadau watatu watatoa...

0

Kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu masuala ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania leo kinaanza kupokea maoni ya wadau katika maeneo tisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dodoma na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia kwa Katibu wa Kikosi Kazi hicho, Sisty Nyahoza, leo wadau watatu watatoa maoni yao katika ukumbi wa Adam Sapi Mkwawa katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam.

Wadau hao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba na Chama cha Madaktari Tanzania (MCT).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesho ni zamu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kanisa la Sabato Tanzania na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso).

Keshokutwa itakuwa zamu ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).

Sisty alisema wadau hao wanakaribishwa kutoa maoni na mapendekezo katika maeneo yanayohusu mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi na mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Alitaja maeneo mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na katiba mpya.

Mwishoni mwa mwaka jana Rais Samia aliagiza kuundwa kwa kikosi kazi kitakachoripoti moja kwa moja kwake kuhusu masuala ya vyama vya siasa ambacho kiliundwa kikiwa na watu 23.

Kazi hiyo ilifanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ambaye aliteua watu 23 kutoka makundi ya wanasiasa, wanazuoni, asasi za kiraia na wanasheria ili kupitia hoja zilizotolewa na wadau wa demokrasia.

Kikosi hicho kinaongozwa na Mwenyekiti, Profesa Rwekaza Mukandala na kimeundwa baada ya kufanyika kwa kikao cha siku tatu kilichowakutanisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kuanzia Desemba 15-17, 2021 jijini Dodoma.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted