Madeleka akabiliwa na kesi ya kuchapisha habari za uongo

Kutokana na kesi hiyo, upande wa mashitaka umeahidi kuleta mashahidi saba na vielelezo vitatu katika kesi hiyo itakayoanza kusikilizwa Mei 18, 2022.

0

Wakili wa kujitegemea Peter Madeleka amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa akikabiliwa na kesi ya kuchapisha habari za uongo mtandaoni kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Kutokana na kesi hiyo, upande wa mashitaka umeahidi kuleta mashahidi saba na vielelezo vitatu katika kesi hiyo itakayoanza kusikilizwa Mei 18, 2022.

Hiyo ni baada ya upande wa mashataka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ya jinai namba 69/2022 na mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH).

Madeleka ambaye ni mkazi wa AICC Kijenge jijini Arusha amefikishwa mahakamani hii leo Mei 5 kwa mara ya kwanza na kusomewa shitaka linalomkabili kisha kusomewa hoja za awali (PH), mbele ya Hakimu Mkazi, Rhoda Ngimilanga.

Madeleka amesomewa shitaka lake na jopo la mawakili watatu Waandamizi wa Serikali, Ester Martin akisaidiana na Mwanaamina Kombakono na Caroline Matemu.

Akimsomea hoja za awali, wakili Kombakono amedai kuwa Madeleka ni wakili ana anakaa AICC Arusha na kwamba aanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha habari za uongo kinyume cha sheria.

Madeleka pia anamiliki akaunti ya Twitter yenye jina la PMadeleka, ambapo Aprili 18, 2022 katika akaunti hiyo kulikuwa na chapisho lililosema “Huyu ndiye Ereneus Mwesigwa Ofisa Uhamiaji anayeratibu njama za kuniua kwenye group la Whatsapp pamoja na maofisa Uhamiaji wenzake.”

Pia April 19, 2022, Ereneus Mwesigwa, baada ya kuona chapisho hilo mtandaoni alikwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi na Aprili 20, 2022 mshtakiwa alikamatwa eneo la hoteli ya Serena na alipelekwa makao makuu ndogo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, iliyopo Dar es Salaam.

Wakili Kombakono alidai kuwa baada ya mahojiano na Polisi, mshtakiwa alipelekwa katika hoteli aliyokuwa amefikia iitwayo Giana iliyopo Kijitonyama ambapo wakiwa katika chumba alichofikia, askari Polisi walifanya upekuzi maoungoni na ndani ya chumba cha mshtakiwa.

“Katika maungo yake mshtakiwa, askari walimkuta na simu aina ya Infinix Note 10 na hapo hati ya upekuzi ilijazwa na kusainiwa na mshtakiwa pamoja na Polisi,” amedia wakili Kombakono.

Pia Madeleka alisafirishwa hadi mkoani Arusha sehemu anayoishi na kufanyiwa upekuzi katika nyumba yake na katioa ofisi yake ambapo walikamata CPU moja aina ya Dell na flashi moja yenye ukubwa wa GB 8.

“Vielelezo hivyo, vilipelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi na baada ya uchunguzi, simu ilionyesha kuwa ndio iliyotumika kurusha maudhui hayo kwenye mtandao wa Kijamii wa Twitter” amedai.

Upande wa mashtaka wamedai kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi saba na vielelezo vitatu na hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashahidi.

Hakimu Ngimilanga baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka alitoa masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa shtaka linalowakabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Ngimilanga alisema mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka Serikali za mitaa watakaosaini dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja.

Masharti mengine ya dhamana ni kwamba wadhamini hao wawe na kitambulisho cha Taifa na wawe ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa wadhamini wake barua walizowasilisha mahakamani hapo zinaonyesha kuwa wadhamini wanatoka Isevya na sio Dar es Salaam.

Hakimu Ngimilanga aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 18, itakapoanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted