Halima na wenzake wafungua kesi mahakamani kupinga kuvuliwa uanachama wa CHADEMA nchini Tanzania.

Tarehe 11 mwezi huu Baraza Kuu la CHADEMA lilitupilia mbali rufaa ya wabunge hao ambao walikuwa wakipinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya chama hicho, na hivyo kumlazimu...

0

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DKt.Tulia Ackson amesema kwa sasa hawezi kutamka kuwa viti 19 vya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliofukuzwa uanachama vipo wazi, kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani.

Dkt. Tulia ameliambia bunge jijini Dodoma kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama.

Amesema kwa kuwa tayari alipokea barua kutoka kwa wabunge hao 19 wakimtaarifu kuwa tayari wamefungua shauri mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama. Hivyo Bunge haliwezi kuingilia mchakato wa mahakama na badala yake linalazimika kusubiri hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wake

“Bunge haliwezi kuingilia mchakato huo mpaka Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi, ninalazimika kutokutangaza kuwa nafasi za viti maalumu 19 vya Chadema viko wazi mpaka pale mahakama itakapokamilisha kazi yake ya kutoa uamuzi” amesema Dk Tulia

Tarehe 11 mwezi huu Baraza Kuu la CHADEMA lilitupilia mbali rufaa ya wabunge hao ambao walikuwa wakipinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya chama hicho, na hivyo kumlazimu Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika kuwasilisha barua kwa Spika kumtaarifu kuhusu jambo hilo ili aendelee na taratibu nyingine.

Hata hivyo pamoja na maamuzi hayo ya chama wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee baadhi yao walionekana kushiriki vikao vya bunge ambapo wengine walipata nafasi ya kuchangia.

Kabla ya maamuzi ya Spika Tulia hii leo wabunge Hawa Subira Mwaifunga na Grace Tendega walipata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza 

Mdee na wenzake, walifukuzwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu ya chama hicho kwa mara ya kwanza , 27 Novemba mwaka juzi na Jumatano iliyopita, Baraza Kuu likaridhia maamuzi hayo.

Katika mkutano wa Baraza Kuu, wajumbe 413sawa na asilimia 97 ya wajumbe 423 waliohudhuria – waliridhia Mdee na wenzake, kufukuzwa uanachama wa Chadema.

Walituhumiwa kwa kupatikana na hatia kwenye makosa kadhaa, ikiwamo kughushi nyaraka za chama, usaliti, uchonganishi, ugombanishi na kisha kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, kinyume na taratibu na maelekezo ya chama.

Mbali na Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine waliovuliwa uanachama, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa baraza hilo, Grace Tendega.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa Katibu Mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Zanzibar.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted