Waandishi 60 wateuliwa kuwania tuzo za EJAT

Tuzo hizo zimepangwa kufanyika Mei 28, 2022 katika ukumbi wa Hoteli ya Serena, Dar es Salaam

0

Waandishi wa habari 60 wameteuliwa kuwania tuzo za za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2021, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Tuzo hizo zimepangwa kufanyika Mei 28, 2022 katika ukumbi wa Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa Tuzo hizo, Kajubi Mukajanga amesema kazi zilizowasilishwa zilikuwa 598  katika makundi 20.

Amesema idadi ya wateule wa EJAT 2021 kwa upande wa wanawake ni 28 ambayo ni asilimia 47, ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu kulinganisha na Tuzo zilizopita, ambapo wanawake walikuwa 26 sawa na asilimia 44 ya walioingia kwenye hatua hii mwaka jana. Wateule wanaume ni 32, sawa na asilimia 53.

Kajubi amesema jopo la majaji saba lililokaa kuanzia Mei 7 mwaka huu lilimaliza kazi yake, Mei 15, 2022.

Amesema jopo hilo la majaji  liliongozwa na Mwenyekiti wake  Mkumbwa Ally. Wajumbe wengine walikuwa Mwanzo Millinga (Katibu), Aboubakar Famau, Mbaraka Islam, Imane Duwe, Beatrice Bandawe, na Rose Haji.

Amesema Majaji hao wameteua jumla ya waandishi 60 ambao kazi zao zimeonekana kuwa bora zaidi na ambao miongoni mwao watapatikana washindi wa EJAT 2021.

Amesema kati ya wateule hao, wateule tisa ni waandishi wa televisheni, 12 vyombo vya mtandaoni, wanane redio na 31 wanaandikia magazeti.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Majaji, Mkubwa Ally amesema, kazi za mwaka huu, zimeonyesha kuwa na kiwango cha juu ukilinganisha na mwaka jana.

“Hii ni pamoja na kiwango cha waandishi wa habari wa vyombo vya mtandaoni kuonesha kukomaa zaidi katika kazi zao na mwamko wa ushiriki katika Tuzo hizo,” amesema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted