Sheria ya Mtoto Na 21 ya mwaka 2009 nchini Tanzania kufanyiwa marekebisho kuakisi mazingira ya sasa.

Mchakato wa marekebisho ya Sheria hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022.

0

Serikali imedhamiria kuifanyia marekebisho Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 na Kanuni zake, ili iweze kuakisi mazingira ya sasa ikiwa ni pamoja na ukatili wa watoto mtandaoni (online child abuse).

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 bungeni mjini Dodoma leo.

Dk Gwajima amebainisha kuwa, ili kutekeleza hilo, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria na kuyawasilisha kwa wadau, ili kutoa maoni ambapo tayari Wizara imeanza kupokea maoni.

Mchakato wa marekebisho ya Sheria hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022.

Aidha serikali imeunda kikosi kazi cha Taifa cha ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni chenye lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wa mitandaoni na kuwasaidia kutumia vifaa vya kieletroniki kwa usahihi na usalama.

Dk Gwajima ameliambia Bunge kuwa katika kukabiliana na aina mpya ya ukatili dhidi ya watoto mitandaoni, kikosi kazi kina jukumu la kuratibu wadau katika serikali na sekta binafsi kuhuisha masuala ya ukatili dhidi ya watoto mitandaoni na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

Pia amesema serikali imeandaa machapisho/majarida ya kufundishia watoto, wazazi na walimu kuhusu ukatili wa watoto mtandaoni.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted