Timu ya Taifa ya Tanzania kuikabili Algeria

Kocha wa Stars Kim Paulsen alisema wataingia uwanjani kwa kuwaheshimu wapinzani kutokana na ubora walionao.

0

Timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars leo inatarajiwa kushuka dimbani kuikabili Algeria katika mchezo wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika Afcon, dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchezo huo Dar es Salaam jana, Kocha wa Stars Kim Paulsen alisema wataingia uwanjani kwa kuwaheshimu wapinzani kutokana na ubora walionao.

Paulsen alisema timu yake imefanya maandalizi mazuri huku wakikumbushana kuwa makini na kuepuka kufanya makosa madogo hasa kwenye mchezo mkubwa kama huo kwa kuwa unaweza kufanya wakaadhibiwa.

“Juzi tumefanya mazoezi na jana pia, tuko tayari na tunajua Algeria ni timu ya kiwango cha juu, ina wachezaji wazuri wenye vipaji na kwa kulitambua hilo tumejipanga vizuri tukiamini utakuwa mchezo wenye ushindani  mkubwa,”alisema.

Alisema wachezaji wake wote wako vizuri isipokuwa Himid Mao ambaye aliumia hivyo atakosekana.

Alisema ili kufanya vizuri wachezaji wake wanahitaji sapoti kutoka kwa idadi kubwa ya mashabiki kujitokeza uwanjani.

Stars inakwenda kukutana na Algeria mchezo wa pili wa kundi F, baada kutoka sare ya bao 1-1 na Niger ugenini nchini Benin huku  wapinzani wao wakiongoza kundi kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mara ya mwisho Stars kucheza na Algeria ilikuwa 2019 kwenye michuano ya Afcon wakiwa kundi moja, walifungwa mabao 3-0.

Pia, waliwahi kukutana katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2015 Stars ikiwa ugenini ilifungwa mabao 7-0 na nyumbani ilitoka sare ya mabao 2-2.

Asilimia kubwa ya kikosi cha Algeria kinacheza nchi mbalimbali za Ulaya na Arabuni wakiongozwa na nahodha wao Riyad Mahrez anayecheza Manchester City.

Hata hivyo, wachezaji wengi wa Taifa Stars ni wazoefu kwani waliwahi kukutana kwenye Afcon ya 2019 kama Mbwana Samatta, Simon Msuva,Aishi Manula na wengine wanaweza kuwaongoza chipukizi  kufanya vyema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted