WHO: Ulaya ‘kitovu’ cha mlipuko wa Monkeypox

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema Jumatano Ulaya inasalia kuwa kitovu cha mlipuko wa Monkeypox duniani, huku visa zaidi ya 1,500 vikiripotiwa katika eneo hilo.

0

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema Jumatano Ulaya inasalia kuwa kitovu cha mlipuko wa Monkeypox duniani, huku visa zaidi ya 1,500 vikiripotiwa katika eneo hilo.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa tayari lilitangaza Jumanne kwamba litafanya mkutano wa dharura wiki ijayo ili kubaini iwapo kutaainisha mlipuko huo kama dharura ya afya ya umma inayohusu mataifa yote.

“Ulaya inasalia kuwa kitovu cha mlipuko huu unaoongezeka huku nchi 25 zikiripoti zaidi ya visa 1,500, au asilimia 85 ya jumla ya visa vyote duniani,” Hans Kluge, mkurugenzi wa kanda wa WHO wa Ulaya, aliambia mkutano na waandishi wa habari Jumatano.

Kanda ya Ulaya ya WHO inajumuisha nchi 53, zikiwemo kadhaa za Asia ya Kati.

“Ukubwa wa mlipuko huu unaleta hatari ya kweli. Kadiri virusi vinavyoenea, ndivyo virusi hivi vinavyopata nguvu zaidi, na ugonjwa huo ukafika katika nchi ambazo hazina ugonjwa huo.” Kluge alisema.

Kufikia miezi michache iliyopita, ugonjwa huo ulikuwa unaenea Afrika Magharibi na Kati pekee.

Kluge alisema kuwa visa vingi vilivyoripotiwa barani Ulaya “vimekuwa vya wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume” lakini pia alionya dhidi ya unyanyapaa.

Alisisitiza “kwamba virusi vya monkeypox haviambatani na kikundi chochote maalum cha magonjwa.”

Mkurugenzi wa WHO wa kanda hiyo pia alionya kuwa hatari inaongezeka kwani majira ya joto yamefika na “utalii, hafla mbalimbali za Pride, tamasha za muziki na mikusanyiko mingine mingi iliyopangwa katika mkoa mzima.”

Steve Taylor, mkurugenzi wa Jumuiya ya European Pride Organiser Association, alisema kuwa baadhi ya matukio 750 ya Pride yalipangwa katika eneo lote la Ulaya na akakaribisha pendekezo la WHO la kutoghairi hafla hizi.

“Cha kusikitisha, baadhi ya wale wanaopinga hafla za Pride na wanaopinga usawa na haki za binadamu tayari wamekuwa wakijaribu kutumia Monkeypox kama uhalali wa wito wa Pride kupigwa marufuku,” Taylor aliwaambia waandishi wa habari.

EU ilitangaza Jumanne kwamba ilikuwa imenunua karibu dozi 110,000 za chanjo kusaidia kukabiliana na mlipuko huo, ingawa WHO haipendekezi chanjo kwa watu wengi dhidi ya Monkeypox.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted