Wanawake vinara wa matumizi ya dawa za kulevya jijini Mwanza

Alisema idadi ya wanawake waliokamatwa katika kipindi kama hicho, mwaka huu ni  22 wakati mwaka jana walikuwa 10.

0

Jeshi la Polisi jijini Mwanza nchini Tanzania limesema idadi ya wanawake jijini humo waotumia dawa za kulevya ni kubwa kulinganisha na idadi ya wanaume

Akisoma taarifa ya mwenendo wa vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya mkoani Mwanza katika utangulizi wa Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Mrakibu wa Jeshi la Polisi,  Denis Rwiza kutoka Ofisi ya Ushirikishwaji wa Jamii wa jeshi hilo, alisema kati ya Februari hadi Mei mwaka huu, idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya kwa wanaume imepungua kulinganishwa na wanawake inayozidi kupanda.

Mrakibu Denis alisema idadi ya wanaume waliokamatwa kwa matumizi ya dawa za kulevya katika miezi hiyo ni 132 kulinganishwa na mwaka jana walikuwa 174.

Alisema idadi ya wanawake waliokamatwa katika kipindi kama hicho, mwaka huu ni  22 wakati mwaka jana walikuwa 10.

“Kwa hiyo kuna ongezeko la watu 12 huku wanaume idadi ikipungua kwa watumiaji 42,” alifafanua.

Alisema kuwa bangi imezidi kuongoza ambapo mwaka huu wamekamata kilogramu 410, ikilinganishwa na kilogramu 207 zilizokamatwa mwaka jana.

“Misokoto ya bangi tumekamata gramu 580 ikilinganishwa na gramu 963.5, sawa na kupungua kwa asilimia 39.9. Miche ya bangi iliyokamatwa ni 1,264 ikilinganishwa na 1,259 iliyokamatwa mwaka jana, sawa na ongezeko la miche mitano ambayo ni asilimia 0.39 iliyokamatwa kwa mwaka 2021,” alisema.

Kwa upande wa mirungi, Mrakibu Denis alisema wamekamata kilogramu 442 kutoka kilogramu 993 zilizokamatwa mwaka jana ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia 10.3, heroine gramu 2.5 ikilinganishwa na gramu 4.5 zilizokamatwa mwaka 2021.

Alisema heroine imepungua zaidi kutokana na udhibiti wa usafirishaji uliofanywa kupitia juhudi za wadau mbalimbali pamoja na Jeshi la Polisi.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya yanatarajiwa kufanyika kitaifa Julai 2 mwaka huu mkoani Dar es Salaam, yakiwa na kauli mbiu ‘Tukabiliane na dawa za Kulevya kwa Ustawi wa Jamii’.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted