Aliyekuwa bosi wa TPA asomewa mashtaka akiwa kitandani Muhimbili

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilihamia kwa muda jana katika hospitali hiyo kwa ajili ya kumsomea Kipande mashtaka yanayomkabili kuanzia saa 8:57 hadi saa 9:08 mchana, likiwamo la...

0

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66), amesomewa mashtaka matatu ya uhujumu uchumi akiwa kitandani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa (MOI), baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilihamia kwa muda jana katika hospitali hiyo kwa ajili ya kumsomea Kipande mashtaka yanayomkabili kuanzia saa 8:57 hadi saa 9:08 mchana, likiwamo la kuisababishia TPA hasara ya shilingi  bilioni 4.2.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Timotheo Mmari mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemalira, alidai kuwa katika shtaka la kwanza Kipande na wenzake wanne walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara kati Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020, jijini Dar es Salaam.

Wenzake ni Peter Gawile (58) Ofisa Rasilimali Watu wa TPA, Casmily Lujegi (65) na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, wote wakazi wa Dar es Salaam.

Alidai kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, mwaka 2015, washtakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia Dola za Kimarekani 1,857,908.04.

Mmari alidai kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi, 2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP).

Ilidaiwa walitangaza zabuni hiyo, bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni kwa kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililoisababishia TPA hasara ya Dola za Kimarekani milioni 1.8 (Sh. bilioni 4.2).

Hakimu Rugemalira alimweleza mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi hadi itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP).

Pia Hakimu Rugemalira alimweleza kwamba kiasi kilichotajwa dhamana yake inaomba Mahakama Kuu na alipowauliza Wakili Mmari kuhusu upelelezi alidai bado haujakamilika.

Hata hivyo, Kipande akiwa kitandani kwa sauti ya chini, aliuliza utaratibu wa kesi ikifunguliwa upelelezi unatakiwa uwe umekamilika, akidai yeye sio mwanasheria ameuliza tu.

Hakimu Rugemalira alimweleza kwamba ni kweli kuna mabadiliko ya sheria yamefanyika kwamba kesi hailetwi mahakamani hadi upelelezi ukamilike, lakini kuna mashtaka yametajwa kwenye hiyo sheria kuwa yanaweza kuletwa kabla ya upelelezi kukamilika yakiwamo mashtaka yanayomkabili.

Kipande alihoji pia atawezaje kwenda Mahakama Kuu kufuatilia dhamana kwa hali yake na Hakimu alimweleza kuwa sio lazima aende yeye amtafute wakili atamwakilisha.

Huku akionyesha tabasamu, Kipande alidai mawakili wana bei kubwa. “Nategemea haki inatendeka na wapelelezi watafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila kula rushwa kwa sababu makosa mengine ni ya kubambikiwa,” alidai.

Hakimu alimweleza maelezo hayo atayatoa wakati wa ushahidi na pia alimwambia washtakiwa wenzake wapo Keko Gerezani, walisomewa mashtaka yao Juni 30, 2022.

Hakimu Rugemalira aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted