Morocco yawafungulia mashtaka wahamiaji baada ya janga la Melilla

Kesi ya wahamiaji 36 wanaoshtakiwa kwa ‘kuingia Morocco kinyume cha sheria,’ ilianza Jumatatu siku chache baada ya jaribio kubwa la kuvuka hadi katika eneo la Uhispania.

0
Waandamanaji wakinyanyua mabango wakishiriki katika maandamano katika mji mkuu wa Morocco Rabat mnamo Julai 1, 2022, wakitaka uchunguzi ufanyike baada ya jaribio kubwa la kuvamia kizuizi kati ya Morocco na eneo la Melilla nchini Uhispania mnamo Juni 24 na kusababisha vifo vya wahamiaji 23. (Photo by AFP)

Kesi ya wahamiaji 36 wanaoshtakiwa kwa ‘kuingia Morocco kinyume cha sheria,’ ilianza Jumatatu lakini ilisitishwa mara moja, mawakili walisema, siku chache baada ya jaribio kubwa la kuvuka hadi katika eneo la Uhispania.

Kesi hiyo ilisikilizwa siku 11 baada ya takriban wahamiaji 23 kufariki wakati wa jaribio kubwa la kuingia katika eneo la Melilla nchini Uhispania kwenye pwani ya kaskazini mwa Morocco.

“Tumeomba kuahirishwa ili kuandaa vyema kesi, kwani mawakili wengine walikuwa wamejiunga na timu ya utetezi,” wakili Khalid Ameza aliambia AFP.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya “kuingia kinyume cha sheria katika eneo la Morocco,” ghasia dhidi ya vikosi vya usalama, kuunda “kundi la watu wenye silaha,” na “kukataa kutii” amri za vikosi vya usalama.

Kesi inayofuata itasikilizwa Julai 12 katika mji wa kaskazini mwa Morocco wa Nador, karibu na Melilla.

Wahamiaji wengine 29, akiwemo mtoto mdogo, wanakesi katika  mahakama huko Nador mnamo Julai 13 kwa mashtaka ya “kujiunga na genge la wahalifu kuandaa na kuwezesha uhamiaji haramu,” Ameza alisema.

Washtakiwa 65 ni miongoni mwa wahamiaji 2,000 ambao mnamo Juni 24 walivamia uzio wa Melilla wenye silaha nzito, moja ya mipaka ya ardhi kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya.

Huku mamlaka ikisema wahamiaji 23 walikufa, mashirika ya haki za binadamu yanasema idadi hiyo ilikuwa angalau 37. Wengi wao wanatoka Sudan na hufika Morocco kupitia Libya na Algeria, licha ya mpaka kati ya nchi hiyo na jirani yake wa mashariki kufungwa rasmi.

Idadi ya vifo hivyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika miaka ya majaribio kama hayo ya wahamiaji wanaotafuta maisha bora barani Ulaya kupitia maeneo ya Uhispania ya Melilla na Ceuta.

Mkasa wa hivi punde ulizua malalamiko ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na ukosoaji mkali usio wa kawaida kutoka kwa Umoja wa Mataifa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted