Pacha mmoja aliyetanganishwa afariki dunia   

Taarifa iliyotolewa na Hospitali hiyo leo Julai 12, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Aminiel Aligaesha imeeleza kuwa hali ya Neema ilibadilika ghafla akiwa katika...

0

Mmoja kati ya watoto pacha waliotenganishwa Julai Mosi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Neema amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu siku ya Jumapili Julai 10, 2022.

Taarifa iliyotolewa na Hospitali hiyo leo Julai 12, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Aminiel Aligaesha imeeleza kuwa hali ya Neema ilibadilika ghafla akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Muhimbili ilifanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao walioungana kifuani Rehema na Neema Julai 1 mwaka huu.

Katika taarifa yake, Aligaesha amesema “Nasikitika kukufahamisha kuwa mtoto Neema ambaye alitenganishwa na mwenzake Rehema amefariki jumapili ya Julai 10 saa 3 asubuhi.

“Akiwa ICU hali yake ilibadikika ghafla, madaktari walijitahidi kurudisha hali yake bila mafanikio na hatimaye kupoteza maisha. Twendelee kumwombea Rehema ambaye bado yupo ICU ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema. Bwana alitoa na Bwana ametoa, jina lake lihimidiwe sana,” ameeleza

Bibi wa Pacha hao Dorica Josiah amesema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa kwani hali ya watoto hao ilikuwa inaimarika tangu walipofanyiwa upasuaji.

“Hizi taarifa zilinichanganya na kuniumiza sana, bado tunaendelea na mipango kuona ni namna gani tutampumzisha Neema, tupo katika wakati mgumu kwa sasa. Muhimbili wametuambia wanaandaa kuhusu mazishi ya mtoto tunasubiri kutoka kwao,” amesema Dorica.

Kabla ya upasuaji Julai Mosi, 2022 watoto hao walichangia mshipa mmoja wa damu unaotoa damu kwenye ini kupeleka kwenye moyo.

Watoto hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kuletwa Muhimbili Novemba mwaka jana, wakiwa na uzito wa kilo saba na sasa wana uzito wa kilo 13.3.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted