Homa ya Ini tishio Afrika

Takwimu za Shirika la Afya Duniani kupitia taarifa ya mwaka 2021 zinaonesha kati ya watu milioni 296 duniani wenye homa sugu ya ini asilimia 66 ya maambukizi hayo...

0

Takwimu za Shirika la Afya Duniani kupitia taarifa ya mwaka 2021 zinaonesha kati ya watu milioni 296 duniani wenye homa sugu ya ini asilimia 66 ya maambukizi hayo yapo barani Afrika.

Katika kupambana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania, imesema utaratibu wa kuwapatia kina mama wajawazito kinga ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mjamzito kwenda kwa mtoto zipo katika hatua za mwisho.

Wakati huohuo takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zinaonesha kuwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B miongoni mwa wachangiaji damu kwa miaka mitatu mfululizo ni asilimia 4.4 kwa mwaka 2018, mwaka 2019 asilimia 5.9, 2020  asilimia 6.1na mwaka 2021 (5.3%).

Hayo yamesemwa leo Julai 28, 2022 na Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu wakati wa akitoa tamko la siku ya maadhimisho ya homa ya ini duniani ambayo ni leo yenye kaulimbiu isemayo ‘Kusogeza huduma za Homa ya Ini jirani na Jamii’.

“Mwaka 2019, watu milioni 296 duniani walikuwa wanaishi na Homa sugu ya Ini aina ya B ambapo asilimia 66 ya maambukizi hayo yalikuwa yanatoka katika Bara la Afrika. Aidha, watu wapatao milioni 58 walikua wanaishi na maambukizi ya Homa sugu ya Ini aina ya C,” amesema Waziri Ummy.

Amesema maambukizi ya homa hiyo aina C nchini kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo takwimu za damu salama kwa wachangiaji yameendelea kuwa ni ya asilimia 2.3.

Amesema ugonjwa wa ini aina ya A na E unaweza kuzuilika kwa kuboresha usafi wa mazingira, utayarishaji wa vyakula katika hali ya usafi na matumizi ya maji safi na salama.

Amebainisha kuwa ugonjwa wa homa ya ini aina ya B, C na D inazuilika kwa kutekeleza afua zote za kuzuia virusi vya VVU/Ukimwi.

“Kwa virusi aina ya B ipo chanjo ambayo hutolewa kwa utaratibu wa kawaida wa utoaji wa chanjo kwa watoto wachanga. Chanjo hii ilianza kutolewa kwa watoto nchini waliozaliwa kuanzia mwaka 2002 (Pentavalent). Kwa kipindi cha mwaka 2021 utoaji wa chanjo ulifikia kiwango cha asilimia 98 ya watoto wote chini yamiaka mitano walipata chanjo ya Pentavalent,” amesema.

Waziri Ummy amesema hakuna chanjo dhidi ya homa ya ini C, D na E.

Hata hivyo amesema chanjo ya watu wazima hutolewa kwa watu walio kwenye makundi hatarishi. “Makundi hatarishi kwenye maambukizi ya aina B na C ni watumishi wa afya, wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, watu wanaojidunga madawa ya kulevya, watu wenye wapenzi wengi, watu wenye magonjwa sugu ya Iini, figo, kisukari na wenye upungufu wa kinga mwilini,” amebainisha.

Waziri Ummy amefafanua kuwa ili kupambana na homa ya ini aina ya B na utaratibu wa kuwapatia mama wajawazito kinga ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto zipo katika hatua za mwisho.

“Wizara pia imekamilisha muongozo wa matibabu ya homa ya ini ambao utatumika kutoa maelekezo ya tiba hiyo nchi nzima ili kumpunguzia mwananchi gharama ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupata tiba hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili”.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted