Hakimu Ndeyekobora aondolewa kusikiliza kesi ya Mfalme Zumaridi

Kuondolewa kwa hakimu huyo huenda kukawa ni majibu ya maombi yaliyowasilishwa Julai 28,2022 na mshtakiwa namba moja katika shauri hilo Mfalme Zumaridi kupitia kwa mawakili wake wakimtaka, Ndyekobora...

0

Hakimu Monica Ndyekobora ameondolewa kusikiliza shauri la Jinai namba 12/2022 linalomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 badala yake shauri hilo litasikilizwa na Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi.

Kuondolewa kwa hakimu huyo huenda kukawa ni majibu ya maombi yaliyowasilishwa Julai 28,2022 na mshtakiwa namba moja katika shauri hilo Mfalme Zumaridi kupitia kwa mawakili wake wakimtaka, Ndyekobora kujiondoa kusikiliza shauri hilo kwa kile walichodai mteja wao hana imani naye huku hakimu huyo akiweka ngumu kujiondoa kwa kile alichodai maombi hayo hayana mashiko.

Hii leo Agosti Mosi 2022, kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusikiliza hoja kutoka kwa mawakili wa utetezi jambo ambalo halikufanikiwa baada ya Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi kupanda mahakamani hapo na kutangaza kwamba shauri hilo limepangwa chini yake kuanzia leo huku akiitaarifu mahamakama kwamba atasikiliza shauri hilo kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 15 mwaka huu.

Bila kutaja sababu za Ndyekobora kuondolewa, Mushi aliagiza upande wa Jamhuri kupeleka mashahidi watatu siku hiyo ili kuendelea na usikilizaji wa ushahidi baada ya shahidi mmoja kati ya 20 wa Jamhuri kumaliza kutoa ushahidi wake chini ya Hakimu Ndyekobora.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Linus Amri aliitaarifu mahakama hiyo kwamba haoni haja ya kuendelea na uwasilishaji wa hoja za upande huo huku akisema hoja hizo zilimlenga Hakimu, Ndyekobora ambaye ameondolewa.

“Kwa sababu kesi hii imepangwa kwako badala ya Ndyekobora basi upande wa utetezi hatuna hoja nyingine ya kuwasilisha. Tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hili,” amesema Amri

Baada ya kuwasikiliza mawakili wa pande zote, Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 15 mwaka huu litakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri.

“Tutasikiliza kesi hii kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 15 mwaka huu. Na kwa kuanzia tutaanza na mashahidi watatu wa Jamhuri maana tuko nyuma ya wakati,” alisema Mushi

Katika hatua nyingine, kesi ya jinai namba 11/2022 inayomkabili Mfalme Zumaridi pekee yenye shtaka la usafirishaji haramu wa binadamu imeahirishwa hadi Agosti 15,2022 baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga kuiambia mahamakama hiyo kwamba upelelezi wake haujakamilika.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted