Tanga Kinara ukusanyaji mapato mikoa ya Tanzania Bara

Waziri Bashungwa amesema kimkoa, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 167.5, ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma Sh bilioni 89.4 na mkoa wa...

0
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, Innocent Bashungwa akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa ametoa taarifa ya mapato kwa mikoa ya Tanzania Bara katika mwaka wa fedha 2021/22 ambapo jiji la Tanga limeongoza kwa kukusanya wastani wa asilimia 113, likifuatiwa na jiji la Dar es Salaam (asilimia 108), Arusha (asilimia 104), Dodoma (asilimia 103), Mwanza (asilimia 100) na Jiji la Mbeya likiwa la mwisho kwa kukusanya wastani wa asilimia 92 ya makisio.

Waziri Bashungwa amesema kimkoa, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 167.5, ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma Sh bilioni 89.4 na mkoa wa Pwani uliokusanya Sh bilioni 48.7.

  “Mkoa wa Rukwa umekuwa wa mwisho kwa kukusanya Sh bilioni 9.4, ukifuatiwa na Katavi Sh bilioni 13.6, na Mkoa wa Simiyu Sh bilioni 14. Mikoa hii pia ina idadi ndogo ya halmashauri ukilinganisha na mikoa mingine,” Waziri Bashungwa amesema.

 Bashungwa amewataka wakuu wa mikoa yote kuongeza nguvu na kufanya vizuri zaidi hususani kwa mkoa wa Dar es Salaam richa ya kuongoza kwa ukusanyaji mapato.

 Kuhusu Halmashauri za Manispaa, Bashungwa ametaja Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuwa imeongoza kwa kukusanya asilimia 125, Kigamboni (asilimia 118), Ubungo (asilimia 118), Moshi (asilimia 117) na Mtwara imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 78 ya makisio ya mwaka.

 Vilevile amesema Halmashauri ya mji wa Mbulu imeongoza kwa kukusanya asilimia 140, ikifuatiwa na Mafinga (asilimia 129), Ifakara (asilimia 125), na halmashauri ya mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 71 ya makisio ya mwaka.

 Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imeongoza baada ya kukusanya asilimia 247, ikufuatiwa na wilaya ya Mlele (asilimia 185) na Morogoro asilimia 158.

 Bumbuli imekuwa wilaya ya mwisho kwa kukusanya asilimia 58 ya makisio ya mwaka, ikufuatiwa na Korogwe (asilimia 67) na Bunda asilimia 70. “Bado mna nafasi ya kufanya vizuri zaidi. Mbulu imekuwa ikikusanya chini ya Sh bilioni 1 na imekuwa ikishika nafasi ya mwisho hata hivyo tathmini ya mwaka uliopita Mbulu imeongoza,” amesema Waziri Bashungwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted