KENYA: Maafisa wanne wa IEBC wapigwa kalamu siku moja kabla ya uchaguzi

Maafisa wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC) wamekamatwa baada ya kupatikana wakifanya mkutano nyumbani kwa muwaniaji wa ubunge

0
Maafisa wa tume ya IEBC katika kituo cha kupigia kura wakiwasaidia wapiga kura (Photo: File)

Maafisa wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC) wamekamatwa baada ya kupatikana wakifanya mkutano nyumbani kwa muwaniaji wa ubunge eneo la Ndhiwa kaunti ya Homa Bay.

Maafisa hao ni afisa wa kituo cha kipigia kura, wasaidizi wake wawili na karana wa tume hiyo. Wanne hao walikuwa wameajiriwa na tume ya IEBC kusimamia vituo viwili katika wadi za Kwabwai na Kanyadoto.

Usimamizi wa IEBC katika kaunti ya Homa Bay umesema wanne hao tayari wameondolewa katika orodha ya maafisa wa IEBC watakaosimamia  uchaguzi wa siku ya Jumanne.

Kwa sasa tume hiyo iko mbioni kuwatafuta watakaofanya kazi katika nafasi hizo huku polisi wakiwa wameanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mkutano huo.

Maafisa wa polisi hata hivyo wamewahakikishia wakenya kuwa wanne hao watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kukiuka sheria za uchaguzi ili kuwa funzo kwa wengine.

Kisa hiki kinajiri siku moja tu baada ya kisa kingine kutokea katika kaunti hiyo ambapo wafuasi wa mgombea wa ugavana kaunti kupitia chama cha ODM Gladys Wanga na mgombea huru Evans Kidero walikabiliana katika kampeni zao za mwisho.

Watu watatu walijeruhiwa katika vurugu hizo za siku ya jumamosi.

Kamishna wa kaunti ya Homa Bay Moses Lilan wakati huo alisema walikuwa wanachunguza kisa hicho kuhakikisha ila hadi kufikia sasa hakuna yeyote aliyekamatwa.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted