Dereva maarufu kwa jina la ‘Ndugu abiria’ kulipwa fidia ya milioni 150 baada ya picha yake kutumiwa kibiashara

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imeiamuru Kampuni ya udalali ya Dexter Insurance kumlipa dereva wa Kampuni ya New Force, Waubani Linyama maarufu kwa jina la 'Ndugu abiria', fidia...

0

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imeiamuru Kampuni ya udalali ya Dexter Insurance kumlipa dereva wa Kampuni ya New Force, Waubani Linyama maarufu kwa jina la ‘Ndugu abiria’, fidia ya shilingi 150 milioni kwa kosa la kutumia picha yake kibiashara bila idhini yake.

Pia mahakama hiyo leo Agosti 10, imetoa zuio la kudumu dhidi ya kampuni ya udalali ya Dexter Insuarance kutoendelea kutumia picha ya Linyama kwenye matangazo yao ya biashara.

Linyama akiwakilishwa na wakili wake, Ferdinand Makore alifungua kesi katika mahakama hiyo akiomba kampuni hiyo ya bima imlipe fidia ya milioni 200 kwa kuituma picha ya mdai huyo kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kujipatia faida au biashara.

Amedai kuwa kampuni hiyo iliandika kwenye ukurasa wake wa Instragram ujumbe uliosema, “Tangazo Tangazo ndugu abiria msiwe na wasiwasi basi letu lina bima ya Dexter Insuarance.”

Alisema kwa tangazo hilo kampuni hiyo ilimgombanisha na mwajiri wake yaani kampuni ya New Force kwa kumwaminisha kuwa aliingia mkataba na kampuni nyingine.

Akitoa uamuzi huo Hakimu Mkazi, Erick Rwehumbiza amesema katika shauri lililofunguliwa na Linyama aliomba alipwe fidia ya shilingi milioni 200 na kampuni hiyo ya udalali kwa kutumiwa picha yake kufanya biashara.

“Ktendo cha kampuni hiyo kutumia picha ya mdai kutangaza biashara na kupata faida ameingilia faragha bila ya ridhaa yake,” amesema Rwehumbiza.

Amesema kutokana na hilo mahakama hii imeamuru kampuni hiyo kumlipa Linyama fidia ya shilingi milioni 150 kwa kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii kwenye ukurasa wa Instagram kwa lengo la kufanyia biashara na kupata faida.

Rwehumbiza amesema pia mahakama hiyo imeamuru kampuni hiyo kila siku inatakiwa kutoa asilimia saba kama riba ya kimahakama siku maamuzi yalipotolewa kuanzia Agosti 10, 2022 hadi mdai atakapolipwa na kampuni hiyo gharama ya shilingi milioni 150 

“Mdai anatakiwa arudishiwe gharama alizotumia kwenye kesi hii,” amesema Rwehumbiza.

Hakimu huyo amesema, Linyama aliyeleta madai yake hayo Julai 16, 2021, ni mwajiriwa wa kampuni ya mabasi ya New Force na picha hiyo iliyosambaa mitandaoni alipigwa mwaka 2019 akiwa anaendesha gari akitokea Sumbawanga kuja Dar es Salaam.

Alipigwa akiwa Mafinga akizungumza kupitia kipaza sauti (microphone) akiwaelezea abiria kuwa atapumzika ili abiria wapate chakula.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted