Mfalme Zumaridi aibua hoja ya ugonjwa Mahakamani

Kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu, Clescensia Mushi imeitwa leo Jumatatu Agosti 15, 2022 kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji...

0

Kesi ya Jinai namba 12/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 84 imelazimika kusimama kwa muda baada ya Zumaridi kuieleza mahakama hajapatiwa matibabu ya majeraha aliyopata kutoka kwa Polisi siku ya ukamataji.

Kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu, Clescensia Mushi imeitwa leo Jumatatu Agosti 15, 2022 kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa mashahidi watatu wa upande wa jamhuri.

Baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo akisaidiana na Deogratius Rumanyika kuieleza mahakama hiyo wako tayari kuendelea na shauri hilo, Zumaridi alinyanyua mkono na kutamka kwamba hayuko tayari kuendelea na shauri hilo leo kwa kile alochodai hajiskii vizuri kiafya.

Baada ya Hakimu, Mushi kumpatia nafasi afafanue tatizo hilo, Zumaridi ameieleza mahakama hiyo pamoja na kushambuliwa na maofisa wa jeshi la Polisi kwa kutumia marungu na fimbo siku ya ukamatwaji lakini hajapatiwa matibabu jambo lililomsababishia uvimbe upande wa kulia mgongoni.

Pia amesema mkono wake wa kulia haufanyi kazi ipasavyo na kudai anaugulia maumivu makali kutokana na kipigo hicho kwa kipindi chote alichokamatwa hadi kufunguliwa mashtaka katika mahakama hiyo bila kupatiwa matibabu.

“Siku ya ukamataji askari Polisi walinipiga virungu kwahiyo humu mifupa yangu inauma sana, Mkono wa kushoto mgongoni nina uvimbe mkubwa kwa sababu sijapata matibabu yoyote,” Mfalme Zumaridi ameiambia mahakama hiyo.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dorcas Akyoo ameeleza kushangazwa na taarifa ya mshtakiwa huyo namba moja katika kesi hiyo.

“Tumeshtushwa na hoja ya mshtakiwa tulikuwa naye kwa mheshimiwa Ndyekobora kulikuwa na kesi nyingine ya kutajwa hakuitaarifu mahakama kuhusiana na tatizo hilo,” amesema Akyoo na kuongeza

“Lakini si hivyo tu, tangu tuanze haya mashauri hakuna siku mshtakiwa ameeleza suala la kupigwa virungu na kuwa na shida ya Mifupa siyo mara ya kwanza anatamka hivyo,” amesema

Akizungumzia suala la ugonjwa wa mteja wake, Wakili wa Utetezi, Steven Kitale ameieleza mahakama hiyo kwamba Jumamosi Agosti 6,2022 alipomtembelea Zumaridi katika gereza la Butimba jijini Mwanza alimweleza Bibi jela hali ya afya ya mteja wake na kumuomba ampatie matibabu ya majeraha hayo.

Kitale amesema hata hivyo ombi hilo halikufanikiwa baada ya Bibi Jela huyo kudai kwamba katika gereza hilo hakuna daktari wa mifupa hivyo hawezi kutibiwa.

“Huu ni ugonjwa hatuwezi kuuongelea maana yeye (Zumaridi) ndiyo anayejisikia vibaya na anamamlaka ya kuzungumzia afya yake anavyojisikia. Na kwa sababu shauri hili linaendelea kwa siku tatu mfululizo huenda magereza ya Butimba ikampatia matibabu,” amesema Kitale

Baada ya pande mbili kuwasilisha hoja hizo, Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Clescensia Mushi ameahirisha shauri hilo kwa muda hadi  atakapotoa uamuzi mdogo wa maombi ya mshtakiwa huyo.

Zumaridi na wenzake walikamatwa Februari 23, 2022 katika mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa jijini Mwanza na kufunguliwa mashtaka mbalimbali ya jinai ikiwemo kufanya kusanyiko bila kibali, kushambulia Maofisa wa Umma na kuzuia maofisa wa serikali kutekeleza majukumu yao.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted