Kesi ya mauaji ya askari polisi yakwama kuendelea ikisubiri upelelezi

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 11/2022, washtakiwa 10 kati ya 24 ni madiwani, yumo pia Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer na wakazi wengine.

0

Washtakiwa katika kesi ya  mauaji ya askari polisi eneo la Loliondo, wilayani Ngorongoro, wameomba kuharakishwa kwa upelelezi kwa madai kuwa shughuli za maendeleo katika baadhi ya maeneo wilayani humo zinakwama kutokana na zaidi ya nusu ya madiwani wake kushtakiwa.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 11/2022, washtakiwa 10 kati ya 24 ni madiwani, yumo pia Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer na wakazi wengine.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili, la kwanza ni njama ya mauaji, ambapo wanadaiwa kupanga njama ya kuua maofisa wa Serikali na maofisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji, wanadaiwa Juni 10,2022 eneo la Ololosokwan,wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Leo, Agosti 17,2022, kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi,Herieth Mhenga ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili Upendo Shemkole huku utetezi ukiwakilishwa na jopo la mawakili wnane wakiongozwa na wakili William Ernest.

Baada ya kesi kutajwa wakili Shemkole, amedai  kuwa upelelezi haujakamilika, ambapo wakili Ernest ameeleza kuwa wana ombi kwa upande wa jamhuri kuharakisha upelelezi wa shauri hilo kwani miongoni mwa washtakiwa hao ni madiwani.

Amedai kuwa kwa kipindi chote walichoshikiliwa shughuli za kimaendeleo zimekwama kwa sababu hawapo kwa ajili ya kuongoza shughuli hizo kwenye maeneo yao.

“Wananchi wanawaongoza kama unavyowaona wanatumia gharama nyingi kufika mahakamani na wanakuja kwenye kesi badala ya kufanya shughuli za maendeleo,”ameeleza wakili huyo

Naye wakili Paul Kisabo, ameeleza kuwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai imeeleza kuhusu upelelezi kukamilika kwa wakati na kuomba mahakama iuagize upande wa jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati ili haki itendeke.

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo,Hakimu huyo alimwagiza Wakili wa Serikali kupeleka suala hilo kwa viongozi wake ili upelelezi ukamilike na kuwa kuondoa malalamiko na sintofahamu na watu hao wataenda kusikilizwa na  Mahakama Kuu ambayo ndiyo ina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni Molongo Paschal, Albert Selembo,Lekayoko Parmwati,Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati,Morongeti Meeki,Kambatai Lulu, Moloimet Yohana,na Joel Clemes Lessonu.

Wengine ni Simon Orosikiria,Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu,Luka Kursas,  Taleng’o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel,Kelvin Shaso Nairoti,Wilsom  Kiling,James Taki,Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30,2022 itakapotajwa tena.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted