Ashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kutengeneza silaha bandia       

Silaha alizokutwa nazo ni aina ya AKA 47 (SMG) 11, Uzgun moja, bastola tano, fulana mbili za kujikinga na risasi mbili zilizotengenezwa kwa kutumia plastiki na mbao.

0

Jeshi la Polisi mkoani Pwani, linamshikilia mtu mmoja mwanaume (32), mkazi wa Sanze Wilaya Kisarawe, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa tuhuma za kukutwa na silaha mbalimbali za kivita ambazo ni bandia

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani, ACP Pius Lutumo, alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa akitengeneza silaha hizo mwenyewe.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 25, majira ya saa 10:30 jioni maeneo ya Sanze Kata ya Kisarawe.

“Kupitia taarifa fiche, tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na silaha hizo, huku akiwa hana kibali cha umiliki wa silaha hizo,” alisema Lutumo.

Alisema kuwa silaha alizokutwa nazo ni aina ya AKA 47 (SMG) 11, Uzgun moja, bastola tano, fulana mbili za kujikinga na risasi mbili zilizotengenezwa kwa kutumia plastiki na mbao.

“Pia alikutwa na redio ya mawasiliano moja ya bandia na alikiri anatengeneza na anatumia kwa matumizi yake,” alisema Lutumo.

Aliwataka wananchi kuishi kwa kufuata misingi ya sheria na kama wanahitaji kutumia silaha kwa namna yoyote ile, wafuate sheria na taratibu zilizowekwa, ili kupata vibali kutoka taasisi husika.

“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika kuhususiana na tukio hilo,”alisema Lutumo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted