Tanzania yaondoa ulazima wa watu kuvaa barakoa baada maambukizi kupungua

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo leo wakati akitoa mrejesho wa tathmini iliyofanyika siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza wizara itoe mwongozo...

0

Serikali ya Tanzania imeondoa ulazima wa kuvaa barakoa isipokuwa pale inapobidi, baada ya nchi kufikia asilimia 60 ya walengwa wa chanjo ya Uviko 19.

Pamoja na hilo imelegeza masharti katika viwanja vya ndege na mipakani huku ikiweka msisitizo urejeshwaji wa afua za unawaji mikono.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo leo wakati akitoa mrejesho wa tathmini iliyofanyika siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza wizara itoe mwongozo kuhusu uvaaji wa barakoa.

“Kadri hali itakavyobadilika tutatoa mwongozo upya kwa sasa tumefanikiwa kuchanja asilimia 60 ya walengwa yaani Watanzania wenye miaka 18 na zaidi na kufikia lengo la kujenga kinga ya jamii sasa tunaweza kuhimili virusi vya uviko 19.

“Kufuatia hilo Serikali inaondoka ulazima wa kuvaa barakoa isipokuwa pale inapobidi. Watakaovaa ni wale wenye mafua ua magonjwa ya mfumo wa hewa ili kuwakinga wenzao …vaa barakoa lakini pia kwenye mikusanyiko ya watu na maeneo yote ambayo yamewekwa huo ulazima …itakubidi uvae.” Amesema Waziri Ummy.

Amesema mpaka kufikia jana ni wagonjwa 7 pekee ndiyo waliolazwa kwa Uviko 19 na kwamba kati yao hakuna aliyekuwa amechanja.

Kutokana na kupungua kwa maambukizi na vifo vitokanavyo na Uviko 19, Serikali ya Tanzania imelegeza baadhi ya masharti katika viwanja vya ndege ikiwemo kuondoa matumizi ya vipima joto na vipimo vya haraka kubaini virusi ‘Rapid test’.

Masharti hayo yatawahusu wasafiri wanaoingia nchini wakiwa na vyeti vinavyothibitisha hawana maambukizi ya Uviko 19 isipokuwa wale ambao hawana watapimwa vipimo hivyo.

“Matumizi ya vipima joto kuchunguza Uviko 19 kwa wasafiri hayo tunaondoa la pili tunasitisha kufanya kipimo cha haraka kwa wasafiri.

“Vyeti vya chanjo tutavitumia na wasio na cheti au uthibitisho wa kwamba amefanya uchunguzi tutaendelea kuwafanyia rapid test.

“Tunaondoa kuwapima watoto chini ya miaka mitano kufanya kipimo cha Rapid test watoto ambao tutawaruhusu kuingia tutaongeza mpaka miaka 12 wanaruhusiwa kuingia nchini bila kipimo chochote wala cheti cha kuonyesha wamepimwa.” amesema Waziri Ummy

Amesema licha ya kupungua kwa maambukizi nchini hatua zitaendelea kuchukuliwa hadi Desemba 2022 mpaka lengo ambalo nchi imepewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) liwe limefikiwa kwa asilimia 70 ya Watanzania wawe wamechanjwa.

Hivi karibuni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa Kizimkazi visiwani Unguja, aliiagiza Wizara ya Afya kufanya tathmini hali ya maambukizi nchini na iwapo wananchi wanalazimika kuendelea kuvaa barakoa au vinginevyo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted