Wadau wa elimu wapinga mtaala wa umilisi Kenya

Wadau wa elimu wanashinikiza mfumo wa 2:6:6:3 kuondolewe na mfumo wa 8:4:4 kurejeshwa mara moja.

0
Waziri wa elimu wa Kenya profesa George Magoha na baadhi ya wanafunzi na wazazi wao.

Katika hotuba yake kwa taifa mara tu alipoapishwa, rais Wiliam Ruto alitangaza kuwa atabuni jopo kazi ambalo litachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu mustakabali wa mfumo wa umilisi nchini Kenya.

Hata hivyo siku mbili baadaye, wadau mbalimbali wamejitokeza wakishinikiza mfumo huo kuondolewe na mfumo wa 8:4:4 kurejeshwa mara moja.

Baadhi ya wabunge wa bunge la kitaifa nchini Kenya wameapa kuhakikisha kuwa mtaala wa umilisi unaondolewa.

Wakizungumza na Mwanzo TV wabunge hao wakiongozwa na John Makali wa Kanduyi, Majimbo Kalasinga wa Kabuchai na mwakilishi wa kina mama kaunti ya Transnzoia Lilian Siyoi, wamesema kuwa mfumo huo unawagharimu wazazi fedha zaidi na haujaboresha viwango vya masomo.

Usema wa viongozi hao umesisitizwa na aliyekuwa katibu mkuu wa muungano wa walimu (KNUT) Wilson Sossion ambaye anadai kuwa  mfumo wa CBC haujawai kutekelezwa nchini Kenya.

Kulingana na Sossion, mfumo wa masomo ambao ulizinduliwa mwaka wa 2017 sio wa umilisi na badala yake ni ule unaozingatia kile mwanafunzi anaweza kufanya baada ya kukamilisha masomo yake.

Sossion anasisitiza kuwa CBC, inalenga kukuza uwezo na ujuzi wa mwanafunzi unaohitajika katika shughuli za kila siku baada ya masomo yake.

“Mfumo unaotekelezwa nchini kwa sasa si wa umilisi na naweza kusema kuwa hatujawai kuwa na mtaala wa CBC katika shule zetu. Walimu vilevile hawafunzi mfumo huo, kile wanafunza ni mtaala unaoangazia matokeo ya mwanafunzi baada ya masomo,” alisema Sossion.

Katibu huyo ni mmoja wa wadau wa Elimu ambao wamekuwa wakiupinga mfumo huo kwa jino na ukucha tangu ulipozinduliwa mwaka wa 2017, kwa misingi kuwa taifa la Kenya halikuwa limeweka miundo msingi ya kutosha kufanikisha utekelezaji wake.

Aidha anasema hatua ya rais William Ruto kutangaza kubuni jopo kazi litakalochunguza na kutoa mapendekezo kuhusu mtaala huo, ina maana kuwa mfumo wa elimu nchini Kenya unakumbwa na matatizo si haba na unahitaji kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.

Baadhi ya wazazi nchini Kenya wamekuwa wakilalama kuwa mfumo huo ulianishwa bila kujumuisha maoni yao na unawagharimu muda na hela zaidi ya ule wa zamani, wengi wakitaka usitishwe.

Hata hivyo hofu yako kuu ni kwamba huenda wanafunzi wengi wa darasa la nane na gradi ya sita wakakosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mapema mwaka wa 2023 kwani wote watafanya mitihani yao ya kitaifa na wanatarajia kuendelea na masomo ya shule za upili.

Lakini mtaalamu wa elimu Tom Nyambeka anatofautia na wanaoshikiza kuondolewa kwa 2:6:6:3 akisema laiti ingepewa muda wa kutoa uhamasisho kwa wazazi na kuwafunza walimu kuhusu mfumo huo wa elimu.

Nyambeka anasisitiza kuwa changamoto kuu katika utekelezaji wa CBC ni kuwa ulizinduliwa bila kuwa na mipango maalum ya utekelezwaji.

“Inasemekana kuwa kuna madarasi ya CBC ya kutosha, ila unapotembelea shule mbalimbali utagundua kuwa pengine hayo ni madarasi yaliojengwa kwenye fikra za wanaopigania mfumo huo ama upo kwenye shule ambazo ni za Kenya lakini hazipo Kenya,” alisema Nyambeka.

Pamoja na hayo yote itabidi wakenya wasubiri mapendekezo ya jopo litakalobuniwa kubaini mustakabali wa mtaala wa umilisi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted