Usilolijua kuhusu mazao ya GMO

Muongo mmoja uliopita uzalishaji na uagizaji wa mazao ya GMO ulipigwa marufuku na serikali ya Kenya kwa misingi kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.

0
Mazao ya GMO

Kufuatia hatua ya serikali kuondoa marufuku ya uzalishaji na uagizaji wa vyakula vilivyokuzwa kisayansi, maarufu GMO, kumekuwa na mjadala na maswali kuhusu vyakula hivyo.

Kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri chini ya uwenyekiti wa Rais William Ruto mnamo Jumatatu, Oktoba 3, serikali iliamua kuanza kutekeleza mapendekezo ya jopokazi lililochunguza kuhusu vyakula vya GMO na usalama wake kwa binadamu.

Muongo mmoja uliopita uzalishaji na uagizaji wa mazao ya GMO ulipigwa marufuku na serikali ya Kenya kwa misingi kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.

Wanaharakati wanaopinga mimea ya GMO nchini Kenya wameonyesha hofu kuwa kuingiza vyakula vya GMO nchini Kenya kutaathiri afya ya wakenya na mazingira ikiwemo ugonjwa wa saratani.

Emmanuel Atamba ni mshirikishi wa Route to Food na mtaalam wa mifumo ya chakula na mifugo, ameiambia Mwanzo TV kuwa kando na athari za kiafya ambazo bado hazijathibitishwa na wataalama wa kiafya hatua hiyo inayapa makampuni makubwa udhibiti mkubwa wa kilimo na uwezo wa kuwanyonya wakulima.

Kulingana na Atamba kampuni inapomiliki haki za zao la GMO wanaweza kuwakataza wakulima kufanya hivi, na kuwalazimisha kununua mbegu mpya kutoka kwa wamiliki kila mwaka.

Atamba anasema hatua hiyo ilichukuliwa na serikali bila kuwahusisha na kupokea maoni ya wakenya hivyo inaonekana kuwa ni uamuzi ambao unawalazimishwa kwa wakenya.

Wakati huohuo anashauri serikali ya Kenya kwanza kukumbatia sera yao ya uongozi ambao ni wa kuimarisha maisha ya wakenya kutoka chini kwenda juu (Bottom up) katika kushughulikia suala la GMO.

Lakini wanasayansi wengi wanasema kuwa vyakula vya GMO ni salama na vinaweza kuliwa kwa urahisi huku wachache wakiwa na wasiwasi navyo.

Sylvester Anami mtaalama wa kiafya anashikilia kuwa vyakula vya GMO havina hatari yeyote ya kiafya akisisitiza kuwa kuna udhibiti uliwekwa kuhakikisha kuwa nyenzo hazina visio.  

Anami ameendelea kusema kuwa hakuna utafiti wa kisayansi uliofanywa na kudhibitisha kuwa vyakula vya GMO vinasababisha Saratani.

“Hakuna ushahidi kwamba GMO inasababisha saratani. Mimea ya GMO haina sumu ila ni salama kwa matumizi ya binadamu. Tunakaribisha lalama za wanaopinga vyakula vya GMO kwa mazungumzo ndiposa kuwarai kuwa vyakula hivyo,” alisema

Lakini GMO ni nini?

Kiumbe chochote kilicho hai ambacho DNA yake imebadilishwa kwa kutumia technolojia ya uhandisi jeni.

Hii inaweza kuwa mmea, mnyama au bakteria na kwa kawaida hufanywa ili kutambulisha sifa inayohitajika katika kiumbe kama vile matunda makubwa au kustahimili ukame.

Hadi kufikia sasa hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba vyakula vilivyobadilishwa vinasaba vina madhara kwa afya ya binadamu.

Watetezi wa uzalishaji wa GMO wanasema vyakula hivi huruhusu wakulima kuzalisha zaidi na kemikali kidogo. Hii inasaidia kulinda mazingira na kufanya kuwa safi kwa muda mrefu.

Hata hivyo, pamoja na faida hii madhara ya muda mrefu ya vyakula vya GMO kwa afya ya binadamu bado hayajulikani.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted