Kesi ya Sabaya, upelelezi kukamilika ndani ya siku 90

Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa mara ya kwanza Juni Mosi mwaka huu wakikabiliwa na mashitaka 7 ikiwemo uhujumu uchumi, ambapo leo...

0

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya imeahirishwa kwa mara ya 10 hii leo, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Kassim Nassir kuieleza mahakama  kuwa upelelezi wake utakamilika ndani ya siku 90.

Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa mara ya kwanza Juni Mosi mwaka huu wakikabiliwa na mashitaka 7 ikiwemo uhujumu uchumi, ambapo leo Oktoba 10 anatimiza siku 132 akiwa mahabusu.

Hata hivyo, Septemba 6 mahakama hiyo iliwaachia huru washitakiwa wanne ambao ni Sylivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey, baada ya kukiri makosa yao na mahakama kuwahukumu kulipa kila mmoja faini ya shilingi 50,000 na fidia ya shilingi milioni 1 kwa mwathirika wa tukio hilo ambaye ni Alex Swai.

Leo Oktoba 10, Wakili wa upande wa utetezi, Hellen Mahuna aliileza mahakama hiyo kuwa kesi inayomkabili mteja wake ambaye ni Sabaya imekaa kwa siku 132 bila upande wa mashitaka kueleza chochote kinachoeleweka zaidi ya kusema upelelezi bado haujakamilika.

Hivyo Wakili Mahuna akaiomba mahakama hiyo iangalie na itumie hekima na muongozo uliotolewa na Mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP) ya kwamba upelelezi unatakiwa ukamilike ndani ya siku 90.

“Kesi hii imekaa kwa siku 132 na upande wa mashitaka hawajatuambia chochote kinachoeleweka zaidi ya kutuambia kwamba upelelezi haujakamilika.

“Wanachokifanya ni kinyume na mwongozo waliopewa na DPP na kwamba wamekuwa hawakamilishi upelelezi kwa wakati na wanamweka mshatkiwa ndani na kumnyima haki zake za msingi,” amesema.

Wakili Mahuna pia ameieleza mahakama hiyo kuwa kama kuna jambo upande wa mashitaka  wanatakiwa kulifanya  kutokana na  mwongozo wa DPP walifanye na wasitegemee kwamba mwongozo umekaa siku 10 tu waangalie siku shauri hilo lilipofikishwa mahakamani.

Kwa upande wake Mwendesha mashitaka wa Serikali, Kassim Nassir ameieleza mahakama hiyo kuwa, kwa kuwa mwongozo huo umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu na kwamba ni siku 10 tu zimepita upelelezi wa shauri hilo utakamilika ndani ya siku 90.

“Tangu mwongozo huo umeanza kutumika Oktoba mosi mwaka huu ni siku 10 tuu zimepita kwa hiyo siku 90 bado hazijaisha ,upelelezi wa shauri hili utakamilika ndani ya siku 90 kama mwongozo unavyoelekeza,” amasema.

Hakimu Mshasha ameiahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 24 mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba mshitakiwa ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa Magereza akisubiri upelelezi utakapo kamilika.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted